
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Mzinga leo Mei 21, 2026 wamesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano yanayolenga kuimarisha ushirikiano katika Utafiti, Teknolojia, Uzalishaji na Usambazaji wa nishati safi ya kupikia.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyofanyika Mkoani Morogoro, Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Mzinga, Mhe. Balozi Luteni Jenerali (Mstaafu), Charles Lawrence Makakala, amesema utekelezaji wa mpango huo utakuwa msaada mkubwa kwa wanawake wa vijijini ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikumbana na changamoto ya kutafuta nishati kwa ajili ya kupikia.
“Akina mama wa vijijini wanapata adha kubwa kutafuta nishati ya kupikia. Madhara ya kiafya wanayoyapata wao pamoja na watoto wao ni makubwa kwa sababu watoto pia hushiriki katika shughuli za maandalizi ya chakula. Hatua hii itasaidia utekelezaji wa sera ya nishati safi lakini pia kuinua ustawi wa jamii na uchumi endelevu,” amesema Makakala.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali (Mstaafu), Jacob Kingu, amesema ushirikiano huo utaongeza uzalishaji wa mkaa mbadala utokanao na mabaki ya mimea pamoja na uzalishaji wa majiko banifu kwa bei nafuu zaidi na hivyo kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy, amesema makubaliano hayo pia yanakwenda kuongeza aina za nishati safi za kutumika zenye gharama nafuu zaidi lengo likiwa kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Mhandisi Saidy amesema kuwa kati ya Watanzania wanne, ni mmmoja tu ndo anatumia nishati safi ya kupikia. Hivyo kupitia ushirikiano huo unaokwenda kuongeza uzalishaji wa mkaa mbadala pamoja na majiko banifu, idadi ya Watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia itakwenda kuongezeka.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mzinga, Brigedia Jenerali Mhandisi Seif Athuman Hamisi, amesema makubaliano hayo yatahusisha maeneo mbalimbali ikiwemo kufanya tafiti za kuboresha matumizi ya majiko na mkaa safi ili kuhakikisha teknolojia hizo zinakidhi mahitaji ya wananchi.








No comments:
Post a Comment