MASWI ASISITIZA UWAJIBIKAJI KWA WATUMISHI WA WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, May 18, 2026

MASWI ASISITIZA UWAJIBIKAJI KWA WATUMISHI WA WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII


Na Okuly Julius, OKULY BLOG , Dodoma


Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Bw. Eliakim Maswi, amewataka watumishi wa Wizara hiyo kuwajibika ipasavyo na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ili kuongeza tija na utendaji kazi ndani ya Wizara.

Bw. Maswi ametoa kauli hiyo Mei 18, 2026 wakati wa mapokezi yake yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara hiyo, Mtumba jijini Dodoma, ambapo alipokelewa na Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Dorothy Gwajima, Naibu Waziri Mhandisi Maryprisca Mahundi, Manaibu Katibu Wakuu Wakili Amon Mpanju na Bi. Felister Mdemu pamoja na viongozi na watumishi mbalimbali wa Wizara hiyo.

Amesema moja ya maeneo anayoyapa kipaumbele ni uwajibikaji wa watumishi huku akisisitiza kuwa kila mtumishi anatakiwa kutathmini mchango wake katika maendeleo ya Wizara hiyo.

Aidha, amesema licha ya Wizara hiyo kuwa miongoni mwa Wizara bora nchini, bado ipo changamoto ya baadhi ya watumishi kushindwa kubadilisha mtazamo na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Sitavumilia uzembe, uongo wala tabia ya kupeleka majungu kwa viongozi. Nataka kuona utendaji wa kazi kwa vitendo badala ya maneno,” amesema Bw. Maswi.

Sambamba na hilo, amewataka watumishi kufika kazini kwa wakati na kufanya kazi kwa bidii akieleza kuwa Serikali imewaamini kwa kuwapatia nafasi hizo huku wananchi wengi wakihitaji ajira.

Pia amesema watumishi wanapaswa kuilinda na kuitumikia Serikali kwa uadilifu kwani changamoto nyingi ndani ya taasisi husababishwa na watendaji kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Aidha, Bw. Maswi amesema atafanya vikao na idara mbalimbali ili kusikiliza changamoto zinazowakabili watumishi huku akiwaagiza kuandika changamoto zao pamoja na sababu zinazowafanya washindwe kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

No comments:

Post a Comment