Mwili wa Baharia Mtanzania, Bw. Mchama Maregesi Mongu, aliyefariki dunia akiwa kazini nchini Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), umewasili nchini Mei 18, 2026 kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.
Mwili huo ulipokelewa na viongozi wa Serikali, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu waliokuwepo uwanjani hapo.
Baharia Mongu alifariki dunia Mei 3, 2026 baada meli ya kuvuta ya VOLANS (tug boat) aliyokuwa akifanya kazi kushambuliwa kwa bomu katika Mlango wa Bahari wa Hormuz ilipokuwa safarini kutoka UAE kuelekea Oman.
Akizungumza baada ya kupokea mwili huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Nahodha Mussa Mandia, ameishukuru Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Konseli Kuu ya Tanzania - Dubai kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na kufanikisha taratibu zilizowezesha kuurejeshwa ngumbani nwa mwili wa marehemu Mongu.
Nahodha Mandia pia ametoa rai kwa wamiliki wa vyombo vya majini kuhakikisha wanazingatia usalama wa watumishi wa Vyombo hivyo kwa kuepuka kupeleka vyombo vyao katika maeneo yenye hatari.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam na mazishi Yake yanatarajiwa kufanyika Mei 21, 2026 katika makaburi ya Makoko, Mwisenge, Musoma mkoani Mara.
Viongozi wengine waliohudhuria mapokezi hayo ni pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Selemani Nyange, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum, pamoja na Katibu Mkuu wa Chama cha Mabaharia Tanzania (TASU), Kapteni Josiah Mwakibuja.









No comments:
Post a Comment