ULEGA ASISITIZA UBORA KATIKA UJENZI WA BARABARA YA DODOMA–CHAMWINO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, May 18, 2026

ULEGA ASISITIZA UBORA KATIKA UJENZI WA BARABARA YA DODOMA–CHAMWINO



Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ameielekeza TANROADS kuhakikisha inamsimamia kwa karibu mkandarasi wa mradi wa upanuzi wa barabara ya Dodoma Mjini–Chamwino Ikulu ili ujenzi huo wa barabara ya njia sita ukamilike kwa viwango vya ubora vinavyoendana na hadhi ya Jiji la Dodoma.

Ulega ametoa maagizo hayo leo Mei 18, 2026 wakati akishuhudia utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 32, hafla iliyofanyika katika Uwanja wa Mashujaa jijini Dodoma.

Mradi huo utakaotekelezwa kwa gharama ya takribani shilingi bilioni 241, umesainiwa kati ya TANROADS kwa niaba ya Serikali na kampuni ya China Railway Construction Engineering Group (CRCEG) ya China kwa lengo la kupanua barabara hiyo kuwa ya njia sita.

Katika maelekezo yake, Ulega amesema barabara hiyo inapaswa kuwa na taa za kisasa, bustani, njia za watembea kwa miguu pamoja na miundombinu ya kisasa itakayolifanya Jiji la Dodoma kuvutia zaidi.

“Tunataka mtu akipita usiku aione Dodoma inavyong’ara. Taa za barabarani lazima ziwe za viwango vya juu,” amesema Ulega.

Aidha, amewataka wataalamu wa usanifu kuzingatia masuala ya usalama kwa kuweka maeneo salama ya kuvuka barabara ili kupunguza ajali zinazoweza kujitokeza katika maeneo mbalimbali ya jiji.

Waziri huyo pia amesema Serikali imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya miundombinu kupitia ujenzi wa barabara na madaraja kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha huduma za usafiri nchini.

Ameeleza kuwa sambamba na mradi huo, Serikali tayari imesaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya mzunguko wa ndani wa Jiji la Dodoma yenye urefu wa kilometa 6.4 inayofadhiliwa na Serikali ya Japan kwa gharama ya yen bilioni 2.78.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Jabir Shekimweri ameishukuru Serikali kwa kutoa shilingi bilioni 19 kwa ajili ya fidia kwa wananchi watakaopisha utekelezaji wa mradi huo.

Shekimweri amesema uongozi wa mkoa utaendelea kushirikiana kwa karibu kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa mafanikio, huku akiitaka Wizara kuzingatia zaidi usalama wa wananchi kwa kujenga vivuko vya juu au chini ya barabara pamoja na kufunga kamera za usalama.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Seleman Kakoso ameipongeza Serikali kwa utekelezaji wa mradi huo na kushauri kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi viporo katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27.

Akitoa taarifa ya mradi huo, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mohamed Besta amesema mradi huo utatekelezwa kwa utaratibu wa Sanifu na Jenga (Design and Build) na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 36, ikiwemo miezi sita ya usanifu pamoja na miezi mitatu ya maandalizi ya awali.



No comments:

Post a Comment