Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi ameshiriki mazishi ya Marehemu Boniface Makene, aliyewahi kuwa Mwandishi wa Habari wa Makamu wa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mohamed Gharib Bilal, yaliyofanyika katika Kijiji cha Mabui Merafuru – Musoma mkoani Mara.
Akitoa salamu za rambirambi kwa waombolezaji, mara baada ya Ibada ya Mazishi iliyofanyika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Agustino Kijiji cha Mabui Merafuru, Makamu wa Rais ametoa pole kwa familia na kwa waombolezaji wote walioguswa na msiba huo.
Amesema Marehemu Boniface Makene atakumbukwa kwa kuwa mshauri mzuri ambaye aliweza kushauri kwa usahihi na kwa nia njema bila kujali mapokeo ya ushauri huo.
Amesema ni muhimu kuwa na Watanzania wengi wa namna hiyo ambao wanakuwa huru kutoa mawazo yao kwa nia njema, bila kuficha ukweli. Amesema uwepo wa utaratibu wa kuwa wakweli na kutoa mawazo kwa nia njema utawezesha kuijenga nchi kwa kiwango kikubwa sana. Makamu wa Rais amesema ni muhimu kila Mtanzania aone anayo nafasi ya kutoa mawazo yake kwa nia njema ya kuijenga nchi.
Halikadhalika, Makamu wa Rais amewashukuru na kuwapongeza Watanzania waishio nje ya nchi yaani Diaspora kwa kazi kubwa waliyofanya kuhakikisha mwili wa Boniface Makene unarejeshwa nyumbani Tanzania. Amewasihi kuendelea kupendana na kushirikiana pamoja na kukumbushana kwamba Taifa lao ni Tanzania. Makamu wa Rais amesema ni furaha kuona jamii ya Diaspora inapofanya mambo mazuri hususani mmoja wao anapopatwa na changamoto.
Awali akitoa mahubiri wakati wa Ibada ya Mazishi, Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Agustino - Mabui Merafuru, Padre Peter Maraga amesema ni vema wanadamu kutumia vipawa walivyopewa na Mungu katika kuwatumikia wanadamu wenzao kama alivyofanya marehemu Makene.
Aidha Padre Maraga, amewasilisha Salamu za Askofu wa Jimbo Katoliki Bunda Mhashamu Simon Masondole ambaye amemkaribisha Makamu wa Rais katika Jimbo hilo na kuahidi kuendelea kumuombea ili kuwa na hofu ya Mungu pamoja na kutimiza majukumu yake kikamilifu.










No comments:
Post a Comment