SERIKALI YAENDELEA KUTAMBUA MCHANGO WA WATU WENYE ULEMAVU KATIKA MAENDELEO YA TAIFA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, May 26, 2026

SERIKALI YAENDELEA KUTAMBUA MCHANGO WA WATU WENYE ULEMAVU KATIKA MAENDELEO YA TAIFA



Na Mwandishi Wetu - Dodoma


Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu, Dkt. James Kilabuko, amesema Serikali ya Tanzania inaendelea kutambua mchango mkubwa wa watu wenye ulemavu katika maendeleo ya Taifa kwa kuweka mazingira wezeshi kupitia sera, sheria, mipango na mikakati mbalimbali.

Amesema Serikali imeendelea kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki, fursa sawa na huduma bora kama wananchi wengine kupitia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2004, Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010 pamoja na kanuni na miongozo mbalimbali inayolenga kuondoa vikwazo vinavyowazuia kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Dkt. Kilabuko amesema hayo leo Mei 26, 2026 jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha utekelezaji wa sera, miongozo na ujumuishaji wa watu wenye ulemavu kilichowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta hiyo.

“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kutambua mchango mkubwa wa watu wenye ulemavu katika maendeleo ya Taifa kwa kuweka mazingira wezeshi kupitia sera, sheria, mipango na mikakati mbalimbali yenye lengo la kuhakikisha wanapata haki, fursa sawa na huduma bora kama wananchi wengine,” amesema Dkt. Kilabuko.

Ameongeza kuwa Tanzania imeridhia Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (CRPD) pamoja na mikataba mingine ya kikanda na kimataifa inayosisitiza haki sawa, utu na ujumuishaji wa watu wenye ulemavu katika maendeleo.

Kwa mujibu wa Dkt. Kilabuko, hatua hiyo inaonesha dhamira ya Serikali kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma katika safari ya maendeleo ya Taifa.

Hata hivyo, amesema pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali bado kuna changamoto mbalimbali zikiwemo uelewa mdogo kuhusu masuala ya ujumuishaji, ukosefu wa huduma jumuishi katika baadhi ya sekta pamoja na changamoto za utekelezaji wa sera na sheria katika ngazi mbalimbali, hali inayohitaji ushirikiano wa wadau wote.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Watu Wenye Ulemavu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu, Wambura Kizito, amesema kikao hicho kinalenga kuwakutanisha wadau wa utoaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu ili kujadili namna bora ya kutekeleza huduma hizo kwa kuzingatia misingi ya ujumuishaji.

Amesema mara nyingi huduma zinazotolewa hushindwa kuwafikia ipasavyo watu wenye ulemavu kutokana na uwepo wa vikwazo vya kimazingira na mawasiliano, hali inayowazuia kushiriki kikamilifu katika mipango mbalimbali ya maendeleo.

“Hivyo tumekutana ili kuona namna ya kushirikiana kuondoa vikwazo hivyo na kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika mipango inayoandaliwa na Serikali,” amesema Kizito.

Naye Meneja wa Programu wa Shirika la Sight Savers Tanzania, Edwin Maleko, akizungumza kwa niaba ya wadau wa mashirika, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuboresha huduma kwa watu wenye ulemavu.

Ameahidi kuwa mashirika hayo yataendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha matokeo chanya yanapatikana katika jamii kupitia utekelezaji wa programu mbalimbali za ujumuishaji.

Kikao hicho kimehudhuriwa na wadau mbalimbali wa utekelezaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu kutoka taasisi na maeneo mbalimbali nchini.







No comments:

Post a Comment