
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, ametoa wito kwa Kampuni ya Mantra Tanzania Limited kuhakikisha inaanza uzalishaji wa madini ya uranium kwa wakati ili Watanzania waweze kunufaika na fursa za kiuchumi zinazotarajiwa kutokana na mradi huo mkubwa wa kimkakati.
Dkt. Kiruswa ametoa kauli hiyo leo Mei 13, 2026 jijini Dodoma alipokutana na kufanya kikao na viongozi wa Kampuni ya Mantra Tanzania, inayotekeleza Mradi wa Mkuju River Uranium Project uliopo Namtumbo mkoani Ruvuma.
Dkt. Kiruswa alikumbusha kuwa mwezi Julai mwaka 2025, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alizindua kiwanda cha majaribio cha kusindika uranium cha Mantra Tanzania, hatua iliyolenga kujaribu teknolojia ya usindikaji pamoja na kukusanya taarifa muhimu kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda kikubwa cha uzalishaji.
Aidha, amesema Serikali haina mpango wa kufuta leseni kubwa ya uchimbaji wa uranium iliyotolewa kwa kampuni hiyo, huku akiitaka kuongeza kasi ya kutafuta mtaji ili shughuli za uzalishaji ziweze kuanza kwa wakati uliopangwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mantra Tanzania Limited, Ilya Shchukin, amesema kampuni hiyo ipo katika hatua za mwisho za kutafuta mtaji kwa ajili ya kuanza ujenzi wa mgodi na kiwanda kikubwa cha usindikaji wa uranium.
Amesema Mantra inaendelea na mazungumzo na taasisi mbalimbali za kifedha kutoka Urusi pamoja na taasisi za fedha za Tanzania ikiwemo Benki ya CRDB na Benki ya NMB ili kufanikisha upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa mradi huo.
Shchukin amesema changamoto kubwa iliyopo ni muda wa leseni ya uchimbaji unaotarajiwa kuisha muda wake Aprili mwaka 2028, hali inayosababisha ugumu kwa baadhi ya taasisi za fedha kutoa mikopo ya muda mrefu kwa ajili ya mradi huo.
Akizungumzia manufaa ya mradi huo kwa wananchi, amesema zaidi ya ajira 4,000 za moja kwa moja zinatarajiwa kuundwa kwa wakazi wa Namtumbo na maeneo jirani, huku zaidi ya kaya 21,000 zikitarajiwa kunufaika kupitia mnyororo wa thamani wa shughuli za mradi huo.
Katika eneo la uwajibikaji kwa jamii, Shchukin amesema Mantra Tanzania imeendelea kuwekeza katika sekta za elimu, afya, mazingira, miundombinu pamoja na uwezeshaji wa vijana na wanawake wanaoishi katika maeneo yanayozunguka mradi huo.
Naye, Meneja wa Mahusiano na Jamii Endelevu wa Mantra Tanzania, Majani Wambura, ameiomba Tume ya Madini kuihuisha leseni ya kampuni hiyo ili kuongeza uwezekano wa kupata mikopo kutoka taasisi za fedha kwa urahisi zaidi.
Wambura amesema, Mradi wa Mkuju River unatarajiwa kuzalisha takribani tani 3,000 za uranium kwa mwaka pindi utakapoanza rasmi uzalishaji, hatua itakayoiweka Tanzania miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa uranium barani Afrika.
Mantra Tanzania Limited ni kampuni tanzu ya Uranium One Group, sehemu ya shirika la nyuklia la Urusi, inayosimamia mradi mkubwa wa uchimbaji na usindikaji wa uranium nchini Tanzania.







No comments:
Post a Comment