Na Okuly Julius,OKULY BLOG,DODOMA
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo amesema Serikali imeendelea kuimarisha usimamizi wa ardhi nchini ambapo hadi Mei 15, 2026 jumla ya migogoro ya ardhi 5,573 imetatuliwa, ekari milioni 3.13 zimerejeshwa kwa wananchi na zaidi ya shilingi bilioni 95.27 zimelipwa kama fidia kwa wananchi waliostahili katika maeneo mbalimbali nchini.
Dkt. Akwilapo amesema hayo wakati akiwasilisha bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka wa fedha 2026/2027 jijini Dodoma.
Amesema kati ya migogoro ya ardhi iliyotatuliwa, migogoro 3,183 ilitatuliwa kupitia kliniki za ardhi huku migogoro 2,390 ikitatuliwa kupitia utaratibu wa kawaida wa kiutawala, hatua ambayo amesema inalenga kuhakikisha wananchi wanapata haki zao na kuendelea kutumia ardhi kwa amani na utulivu.
Aidha, amesema Serikali imeanza utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Kudhibiti Migogoro ya Ardhi Nchini ulioandaliwa kwa kushirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wakulima, wafugaji, wawekezaji pamoja na mamlaka za hifadhi kwa lengo la kupata suluhisho la kudumu la migogoro ya ardhi nchini.
Katika hatua nyingine, Dkt. Akwilapo amesema Wizara imeendelea kuandaa na kusajili hati na nyaraka mbalimbali za kisheria ambapo hadi Mei 15, 2026 jumla ya hatimiliki 107,683 zimesajiliwa sawa na asilimia 21.54 ya lengo, huku hati za hakimiliki ya kimila 99,762 zikiandaliwa na kusajiliwa sawa na asilimia 19.19 ya lengo.
Amesema Wizara pia imefanikiwa kuandaa vyeti vya ardhi ya kijiji 148 sawa na asilimia 148 ya lengo pamoja na hati za sehemu ya jengo 914 sawa na asilimia 91.4 ya lengo.
“Jumla ya miamala ya hatimiliki na nyaraka za kisheria 137,681 zimesajiliwa sawa na asilimia 137.68 ya lengo lililowekwa,” amesema Dkt. Akwilapo.
Kwa upande wa usimamizi wa masharti ya umiliki wa ardhi, Waziri huyo amesema Wizara ilifanya ukaguzi wa viwanja na mashamba 2,503 ambapo wamiliki 932 walibainika kukiuka masharti ya umiliki huku milki 15 zikifutwa na hatua za kisheria kuendelea dhidi ya wamiliki wengine 917.
Amesema Serikali itaendelea kufanya uhakiki wa viwanja na mashamba ili kuhakikisha wamiliki wa ardhi wanazingatia masharti ya umiliki ikiwemo kuendeleza maeneo yao na kulipa kodi ya pango la ardhi kwa wakati.
Kuhusu uwekezaji, Dkt. Akwilapo amesema kupitia Kamati ya Kitaifa ya Ugawaji Ardhi, Wizara imepokea na kuidhinisha maombi 333 ya ardhi ya uwekezaji yenye ukubwa wa hekta 45,371.24.
Amesema Serikali imeendelea kuboresha huduma za ardhi kwa wawekezaji kupitia Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) pamoja na kuongeza Makamishna Wasaidizi wa Ardhi katika mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam na Mwanza ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Wizara imepanga kuandaa na kusajili hatimiliki 200,000, hati za hakimiliki ya kimila 300,000, kushughulikia migogoro ya ardhi 4,000 kiutawala pamoja na kutenga hekta 5,000 za ardhi kwa ajili ya uwekezaji.
Dkt. Akwilapo ametoa rai kwa wananchi kuhakikisha wanamiliki na kuendeleza ardhi zao kisheria ili kuepuka migogoro na kuwawezesha kutumia ardhi kama nyenzo ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.


No comments:
Post a Comment