TABORA YAFUNGUA MILANGO YA UWEKEZAJI MADINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, May 16, 2026

TABORA YAFUNGUA MILANGO YA UWEKEZAJI MADINI


Na Mwandishi Wetu - Tabora


Serikali imewataka wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika sekta ya madini mkoani Tabora ili kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kuinua kipato cha wananchi, kufuatia uwepo wa rasilimali nyingi za madini ambazo bado hazijatumika ipasavyo.

Akizungumza mkoani humo, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tabora, Fatuma Kyando, amesema mkoa huo ni miongoni mwa maeneo yenye utajiri mkubwa wa madini nchini ukiwa na dhahabu, vito, chuma, chokaa pamoja na madini mengine yenye thamani kubwa kiuchumi, hali inayotoa fursa pana za uwekezaji katika uchimbaji, uchenjuaji na uongezaji thamani wa madini.

Amesema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia mitaji mipya, huku akisisitiza kuwa uwekezaji unaozingatia sheria, kanuni na miongozo ya nchi utawezesha wananchi na Taifa kunufaika zaidi na rasilimali hizo.

Amewataka wawekezaji kuchangamkia fursa za utafiti, uchimbaji, uchenjuaji, uuzaji na uongezaji thamani wa madini.

Kyando amesema bado kuna upungufu wa mitambo ya kisasa ya uchimbaji na uchenjuaji madini, akibainisha kuwa kwa sasa mkoani Tabora kuna mitambo minne pekee inayomilikiwa na sekta binafsi, kiwango ambacho hakikidhi mahitaji ya wachimbaji waliopo.

Kutokana na hali hiyo, amewahimiza wawekezaji kuwekeza katika teknolojia za kisasa zitakazoongeza ufanisi wa uzalishaji, kuboresha usalama migodini na kuongeza mapato kwa wachimbaji pamoja na Serikali.

Ameongeza kuwa eneo la uongezaji thamani lina fursa kubwa zaidi kupitia uwekezaji katika uchakataji wa mawe kwa ajili ya utengenezaji wa tiles, kokoto, paving blocks na bidhaa nyingine za ujenzi, hatua itakayochochea viwanda vya ndani na kuongeza thamani ya madini kabla ya kuuzwa.

Aidha, amesema bado kuna maeneo mengi yenye madini ambayo hayajafanyiwa utafiti wa kina, hivyo uwekezaji katika tafiti za madini unahitajika ili kugundua maeneo mapya ya uchimbaji na kupanua wigo wa shughuli za madini mkoani humo.

Kyando pia amesisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa maabara ya kisasa ya upimaji wa sampuli za madini ndani ya Mkoa wa Tabora ili kupunguza gharama na muda kwa wachimbaji wanaolazimika kufuata huduma hizo nje ya mkoa.

Amehitimisha kwa kuzitaka kampuni na wawekezaji binafsi kutumia fursa zilizopo katika biashara na huduma mbalimbali zinazohusiana na sekta ya madini, akieleza kuwa hatua hiyo itaimarisha uchumi wa mkoa wa Tabora na kuongeza mchango wa sekta ya madini katika maendeleo ya Taifa.

No comments:

Post a Comment