TANI 29 ZA KRATOM ZANASWA TANZANIA KWA MARA YA KWANZA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, May 29, 2026

TANI 29 ZA KRATOM ZANASWA TANZANIA KWA MARA YA KWANZA



Na Okuly Julius, OKULY BLOG , DODOMA



Serikali imekamata tani 1,017.26 za bangi, tani 29.52 za dawa mpya ya kulevya aina ya Kratom na kutaifisha mali zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 3.3 katika operesheni mbalimbali za kudhibiti dawa za kulevya zilizofanyika nchini mwaka 2025.

Hayo yameelezwa Mei 29,2026 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba Kabudi, wakati akitoa taarifa ya hali ya dawa za kulevya nchini kwa mwaka 2025.

Kabudi amesema pamoja na bangi, Serikali pia ilikamata tani 26.36 za mirungi, kilogramu 907.18 za methamphetamine, kilogramu 672.23 za heroin na kilogramu 4.89 za cocaine kupitia operesheni zilizofanywa kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.

Amesema kwa mara ya kwanza nchini, Serikali ilifanikiwa kukamata tani 29.52 za dawa aina ya Kratom iliyokuwa imeingizwa nchini kwa kificho ikidaiwa kuwa mbolea.

“Ushirikiano ni silaha muhimu katika vita dhidi ya dawa za kulevya kwani mafanikio ya kweli yanahitaji juhudi za pamoja kati ya Serikali, wadau na wananchi,” amesema Kabudi.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, mafanikio hayo yametokana na kuimarishwa kwa operesheni za udhibiti mipakani, bandarini, viwanja vya ndege na katika njia mbalimbali zinazotumiwa kusafirisha dawa za kulevya.

Kabudi amesema mwaka 2025 jumla ya mashauri 1,124 ya dawa za kulevya yalifunguliwa katika mahakama mbalimbali nchini huku mashauri 1,373 yakitolewa hukumu na Jamhuri kushinda mashauri 1,058.

Aidha, amesema Serikali iliendelea kutoa huduma za tiba na utengamao kwa waraibu wa dawa za kulevya ambapo watu 85,425 walipata huduma hizo kupitia hospitali za rufaa, kliniki za MAT na nyumba za upataji nafuu.

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na vyombo vya dola pamoja na wananchi kuhakikisha biashara na matumizi ya dawa za kulevya vinadhibitiwa ili kulinda nguvu kazi ya taifa na usalama wa jamii.



No comments:

Post a Comment