Na Mwandishi Wetu, Zimbabwe
Tanzania imeendelea kung’ara katika ukanda wa Kusini mwa Afrika baada ya kutajwa kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa mifumo madhubuti ya usimamizi wa maafa, hatua inayozifanya nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kujifunza kupitia uzoefu wake.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya wakati akimwakilisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Mhe. Balamagamba Kabudi wakati wa Mkutano wa Sita wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri Wanaohusika na Usimamizi wa Maafa kwa nchi wanachama wa SADC unaofanyika mjini Masvingo, Zimbabwe.
Amesema Tanzania imefanikiwa kuimarisha mifumo ya kuzuia, kupunguza madhara, kujiandaa na kurejesha hali baada ya maafa kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa katika sekta ya uratibu wa maafa nchini.
Kwa mujibu wa Mhe. Mmuya amesema moja ya mafanikio makubwa ni kuanzishwa kwa Kituo cha Ufuatiliaji wa Mwenendo wa Majanga na Tahadhari ya Mapema (National Emergency Operation and Communication Center Situation Room), ambacho kinafanya kazi saa 24 kila siku kufuatilia na kuchambua taarifa za majanga.
“Kwa kupitia kituo hiki, Serikali imeweza kupata taarifa za mapema kuhusu majanga yanayoweza kutokea, kufanya uchambuzi wa madhara na kuweka mikakati ya haraka ya kukabiliana nayo,” alisema Mhe Mmuya
Aliongeza kuwa matumizi ya teknolojia ya kisasa katika ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu za wakati halisi yamechangia kuongeza ufanisi wa maamuzi na kurahisisha utoaji wa taarifa rasmi kwa wananchi kuhusu namna ya kujiandaa dhidi ya maafa.
“Tunatumia takwimu za sasa na za zamani kutabiri hatari zinazoweza kujitokeza, jambo ambalo linaisaidia Serikali kupanga kwa usahihi hatua za kurejesha hali na kuendelea kulinda maisha ya wananchi,” alisisitiza.
Aidha, aliwaalika wajumbe kutoka nchi wanachama wa SADC kutembelea Tanzania ili kujionea namna mifumo hiyo inavyofanya kazi pamoja na ubunifu unaotumika katika usimamizi wa maafa.
Mkutano huo wa siku nne umezikutanisha nchi 16 wanachama wa SADC pamoja na wataalamu wa kitaifa na mashirika ya kimataifa kujadili utekelezaji wa programu za kikanda za usimamizi wa maafa na namna ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda.
Pamoja na mambo mengine, mkutano huo unatarajiwa kuwa jukwaa muhimu kwa mawaziri na washirika wa maendeleo kujadili uwekezaji katika sekta ya usimamizi wa maafa kwa lengo la kujenga ustahimilivu wa kikanda dhidi ya majanga mbalimbali yanayoendelea kujitokeza duniani.







No comments:
Post a Comment