
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Waziri wa Maliasili na Utalii,Dkt. Ashatu Kijaji, amesema Tanzania imeendelea kupata mafanikio makubwa katika Sekta ya Maliasili na Utalii ambapo idadi ya watalii imeongezeka hadi kufikia milioni 5.9 mwaka 2025, hatua iliyochochea ongezeko la mapato ya fedha za kigeni pamoja na kuimarika kwa hadhi ya nchi kimataifa.
Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni, Dkt. Kijaji amesema mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais katika sekta ya utalii, uhifadhi na miundombinu ya huduma.
Amesema idadi ya watalii imeongezeka kutoka watalii 5,360,247 mwaka 2024 hadi kufikia watalii 5,935,561 mwaka 2025 sawa na ongezeko la asilimia 10.7. Kati yao, watalii wa kimataifa wameongezeka kwa asilimia 7.1 kutoka milioni 2.14 hadi milioni 2.29 huku watalii wa ndani wakiongezeka kwa asilimia 13.1 kutoka milioni 3.21 hadi milioni 3.64.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, Tanzania pia imeendelea kufanya vizuri katika mizania ya utalii duniani ambapo taarifa za zimeonyesha kuwa nchi imeshika nafasi ya 11 duniani kwa ongezeko la wageni wa kimataifa ikilinganishwa na kipindi cha kabla ya janga la UVIKO-19 mwaka 2019.
Aidha, mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 3.9 mwaka 2024 hadi dola bilioni 4.4 mwaka 2025 sawa na ongezeko la asilimia 12.82, hatua iliyoifanya sekta ya utalii kuwa ya pili kwa kuingiza fedha za kigeni nchini baada ya sekta ya madini.
Katika hatua nyingine, Tanzania imeendelea kung’ara kimataifa baada ya kushinda tuzo mbalimbali za utalii duniani kupitia tuzo za ambapo Tanzania ilitangazwa kuwa Nchi Bora ya Utalii wa Safari Duniani kwa mwaka 2025 kwa mara ya tatu mfululizo.
Pia, ilishinda tuzo ya Hifadhi Bora Duniani huku Zanzibar ikitajwa kuwa eneo bora kwa mikutano na matukio ya biashara.
Waziri Kijaji amesema Serikali pia imeendelea kuimarisha miundombinu ya utalii kwa kukamilisha ujenzi wa viwanja vya ndege vitatu ndani ya hifadhi za taifa pamoja na kukarabati viwanja vingine nane katika maeneo mbalimbali ya utalii nchini.
Aidha, kilomita 3,757.92 za barabara pamoja na kilomita 523.14 za njia za watembea kwa miguu zimejengwa na kukarabatiwa katika maeneo yaliyohifadhiwa ili kuboresha upatikanaji wa vivutio vya utalii na kuongeza uzoefu kwa wageni.
Katika eneo la uhifadhi, Wizara imefanikiwa kukamilisha sensa ya kitaifa ya wanyamapori iliyofanyika kwa kutumia fedha za ndani kwa mara ya kwanza, hatua iliyosaidia kubaini mwenendo wa ongezeko la wanyamapori na kuimarisha mikakati ya uhifadhi endelevu.
Sekta ya ufugaji nyuki nayo imeendelea kufanya vizuri ambapo kiwango cha asali kinachouzwa nje ya nchi kimeongezeka kutoka tani 951.6 mwaka 2024 hadi tani 1,596.8 mwaka 2025 sawa na ongezeko la asilimia 67.85 huku thamani ya mauzo ikiongezeka kutoka shilingi bilioni 11.4 hadi bilioni 19.2.
Katika mafanikio mengine, Tanzania imechaguliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Urithi wa Dunia ya kwa kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2025 hadi 2029, hatua inayothibitisha kuimarika kwa hadhi ya nchi katika uhifadhi wa maeneo ya urithi wa dunia.
Wizara pia imekamilisha na kuzindua Makumbusho ya Jiopaki ya Ngorongoro-Lengai yaliyopo Karatu mkoani Arusha, hatua inayotarajiwa kuongeza utalii wa jiolojia, tafiti za kisayansi pamoja na ajira kwa wananchi wa maeneo jirani.
Sambamba na hayo, Serikali imeendelea kufanya mageuzi ya kidijitali kupitia maboresho ya mfumo wa MNRT Portal ili kurahisisha utoaji wa huduma mbalimbali za utalii ikiwemo leseni, vibali vya kuingia hifadhini na huduma za malazi kwa njia ya kielektroniki.

No comments:
Post a Comment