TARURA NANYUMBU YAKAMILISHA UJENZI DARAJA LA MAWE LA SOMOE ISSA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, May 28, 2026

TARURA NANYUMBU YAKAMILISHA UJENZI DARAJA LA MAWE LA SOMOE ISSA



Na Mwandishi Wetu - Nanyumbu, Mtwara


Wananchi wa kijiji cha Chiuve kata ya Nangomba wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara sasa wamepata suluhu ya kudumu ya mawasiliano baada ya kukamilika kwa ujenzi wa daraja katika mto Masyalele.

Hayo yamesemwa na Meneja wa TARURA wilaya ya Nanyumbu, Mhandisi Dickson Mkokota wakati wa ziara ya kutembelea miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara katika wilaya hiyo.

Amesema ujenzi wa daraja hilo lililojengwa katika barabara ya Chiuve-Kalipinde umetekelezwa na Mkandarasi Central Highway kwa gharama ya shilingi 120,560,360 na umekamilika kwa asilimia 100.

Mhandisi Mkokota ameongeza kuwa kabla ya ujenzi wa daraja hilo wananchi wa vijiji vya Chiuve na Kalipinde walikuwa wanatumia kivuko aina ya "drift" ambacho wakati wa mvua walikuwa wanapata shida kuvuka kutoka upande mmoja kwenda upande wa pili kwa ajili ya kupata huduma za kijamii na kiuchumi kama vile hospitali na masoko.

"Manufaa makubwa yaliyopatikana kwenye mradi huu ni watu wamerahishiwa kuvuka katika eneo hili la mto", amesema.

Kwa mujibu wa Mhandisi Mkokota daraja hilo limepewa jina la Somoe Issa kwa sababu kabla ya ujenzi wa daraja alitokea mama mmoja mjamzito kutoka Kijiji cha Chiuve kwenda kujifungua katika hospitali ya wilaya ya Mangaka na kwa bahati mbaya alipofika katika eneo hilo alikuta maji yamejaa na kushindwa kuvuka na kujifungua mtoto ambaye amepewa jina la Somoe Issa hivyo wananchi wa kijiji hicho walipendekeza daraja hilo kuitwa Somoe Issa.

Kwa upande wake, Bi. Ashura Hamis ambaye ni mama wa mtoto Somoe Issa mkazi wa kijiji cha Chiuve amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaondolea changamoto hiyo ya muda mrefu.

"Namshukuru sana mama Samia na serikali yake kwa hili lililofanyika na kwa wamama wenzangu ambao tumejifungulia hapa.
Nashukuru kwa kupewa jina la mwanangu daraja hili Somoe Issa", ameeleza.

Naye, Bw. Rajabu Chakubanga mkazi wa Mangaka Kilimahewa ambaye ni mkulima amesema ukosefu wa kivuko katika eneo hilo ilikuwa ni changamoto kubwa kwao hasa wakati wa kusafirisha mazao yao kutoka mashambani lakini kwa sasa wanashukuru kwani hata gharama za usafirishaji zimepungua.


No comments:

Post a Comment