WIZARA YA ARDHI YAOMBA BAJETI YA SHILINGI BILIONI 210.2 KWA MWAKA 2026/2027 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, May 28, 2026

WIZARA YA ARDHI YAOMBA BAJETI YA SHILINGI BILIONI 210.2 KWA MWAKA 2026/2027



Na Okuly Julius ,OKULY BLOG , DODOMA


Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeomba Bunge kuidhinisha jumla ya shilingi bilioni 210.2 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli na miradi mbalimbali ya Wizara hiyo pamoja na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi katika mwaka wa fedha 2026/2027.

Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo amesema kati ya fedha hizo, shilingi 100,224,553,000 zimeombwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambapo shilingi 61,134,550,000 zitatumika kulipa mishahara ya watumishi wa Wizara na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi.

Aidha, amesema shilingi 39,090,003,000 zimetengwa kwa ajili ya matumizi mengineyo ya kawaida ili kuwezesha utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kiutendaji katika sekta ya ardhi na maendeleo ya makazi.

Kwa upande wa miradi ya maendeleo, Waziri huyo amesema jumla ya shilingi 110,034,962,000 zimepangwa kutumika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayolenga kuboresha usimamizi wa ardhi, upangaji matumizi bora ya ardhi pamoja na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Amefafanua kuwa kati ya fedha za maendeleo, shilingi 44,132,469,000 ni fedha za ndani huku shilingi 65,902,493,000 zikiwa ni fedha za nje kutoka kwa washirika wa maendeleo.

Dkt. Akwilapo amesema bajeti hiyo inalenga kuwezesha Wizara kutekeleza vipaumbele vyake ikiwemo kuimarisha usimamizi wa ardhi, kuongeza upimaji wa maeneo, kutatua migogoro ya ardhi, kuboresha mipango miji pamoja na kuendelea kuimarisha mifumo ya utoaji huduma kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment