ASILIMIA 97 YA VIJIJI NCHINI VYAPIMWA, WIZARA YA ARDHI YAONYA UVUNJIFU WA HAKI ZA ARDHI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, May 28, 2026

ASILIMIA 97 YA VIJIJI NCHINI VYAPIMWA, WIZARA YA ARDHI YAONYA UVUNJIFU WA HAKI ZA ARDHI

 































































































































































































Na Okuly Julius,OKULY BLOG, DODOMA


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo amesema Serikali imefikia hatua kubwa katika upimaji wa mipaka ya vijiji nchini ambapo hadi Mei 15, 2026 jumla ya vijiji 11,996 kati ya vijiji 12,333 vilivyopo nchini tayari vimepimwa.

Dkt. Akwilapo amesema hayo bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026, Wizara ilipanga kuhakiki na kupima mipaka ya vijiji 100 kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa mipaka ya kiutawala na kupunguza migogoro ya ardhi vijijini.

“Hadi tarehe 15 Mei, 2026 mipaka ya vijiji 54 imehakikiwa na kuhuishwa huku vijiji 189 vikifanikiwa kupimwa,” amesema Dkt. Akwilapo.

Ameeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2026/2027, Wizara itaendelea kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI pamoja na wadau wa maendeleo kuhakiki, kuhuisha na kupima mipaka ya vijiji 226 ili kukamilisha zoezi hilo katika maeneo yaliyosalia.

Hata hivyo, Waziri huyo amesema Wizara imeendelea kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi dhidi ya baadhi ya Serikali za Vijiji kuhusu kuathiriwa kwa haki zao za ardhi baada ya kubainishwa kwa mipaka ya vijiji.

Kutokana na hali hiyo, Dkt. Akwilapo amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kuheshimu haki za ardhi za wananchi wakati wa utekelezaji wa shughuli za upangaji na upimaji wa mipaka ili kuepuka kuibua migogoro mipya ya ardhi.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia zoezi hilo kwa karibu ili kuhakikisha wananchi wanalindwa na kunufaika na matumizi bora ya ardhi kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

No comments:

Post a Comment