WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania wabadili mtazamo kuhusu utunzaji na uhifadhi wa mazingira na kwa kila moja kuona ni suala lake badala ya kuliona ni jambo la taasisi za usimamizi wa mazingira pekee.
“Uhifadhi wa mazingira si suala la nadharia wala kaulimbiu bali ni jambo la msingi kwa uhai wa binadamu, maendeleo ya uchumi na ustawi wa Taifa. Watanzania tunapaswa tubadili mifumo ya maisha na shughuli za kiuchumi ili kulinda mazingira kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo,” amesema.
Dkt. Mwigulu amesema hayo leo (Alhamisi, Mei 28, 2026) wakati akifungua Kongamano la Kitaifa la Wadau wa Mazingira pamoja na maadhimisho ya miaka 40 ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) yaliyofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Amesema madhara ya uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi sasa yanaonekana wazi katika maeneo mbalimbali nchini na duniani na kwamba kuna ulazima wa jamii kubadili namna ya matumizi ya ardhi, uzalishaji na matumizi ya rasilimali ili kuhakikisha mazingira yanaendelea kuwa salama na endelevu.
“Uhifadhi wa mazingira si jambo la kaulimbiu. Ni jambo halisia. Ni jambo linaloishi. Uhai wetu unategemea mazingira. Mazingira yanaweza kuendelea bila binadamu, lakini binadamu hawezi kuishi bila uwepo wa mazingira,” alisema Dkt. Mwigulu.
Aidha, Waziri Mkuu alisema ongezeko la watu, shughuli za kiuchumi na matumizi holela ya ardhi vimeongeza ushindani wa matumizi ya rasilimali, hali inayohitaji matumizi ya teknolojia za kisasa na mbinu endelevu katika sekta za kilimo, ufugaji, ujenzi na uzalishaji.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu alisifu juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kusimamia ajenda ya mazingira na nishati safi ya kupikia akieleza kuwa Serikali imeendelea kuwekeza katika miradi ya umwagiliaji, nishati safi na reli ya kisasa (SGR) ambayo inalenga kupunguza athari za uharibifu wa mazingira.
“Mheshimiwa Rais ameonesha mfano mkubwa wa namna ya kubadili namna ya kufanya kwa mazoea ambapo ameongeza bajeti ya umwagiliaji na kuwezesha wakulima kuvuna mara tatu kwa mwaka. Alikuta miradi 13 na sasa kuna zaidi ya miradi 780. Hizi ni jitihada za makusudi za kuwainua Watanzania,” amesema.
Pia aliwataka wananchi walione suala la mazingira kuwa ni wajibu wa kila mmoja badala ya kuliacha kwa taasisi za serikali pekee, huku akiitaka NEMC kuendelea kuimarisha elimu ya mazingira kuanzia ngazi ya familia, shule na jamii kwa ujumla. “Jukumu la uhifadhi wa mazingira ni la kila mmoja wetu na hatupaswi kuliacha jukumu hilo mikononi wa Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pekee yake.”
Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika uchumi wa kijani, matumizi ya teknolojia safi, nishati jadidifu, uchumi wa mzunguko, pamoja na mifumo madhubuti ya usimamizi wa taka na udhibiti wa uchafuzi wa mazingira
“Katika kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Tanzania inalenga kuwa Taifa lenye uchumi shindani, jumuishi na wenye ustahimilivu dhidi ya changamoto za mazingira na mabadiliko ya tabianchi. Tutaendelea kuimarisha matumizi ya sayansi, tafiti na teknolojia katika kufanya maamuzi yanayohusu usimamizi wa mazingira,” amesisitiza.
Katika kongamano hilo, Waziri Mkuu pia alizindua Mfumo wa Kidijitali wa Ufuatiliaji wa Uchafuzi wa Mazingira Tanzania (TOCEMS - Tanzania Online Continuous Emission Monitoring System) ambao utawezesha ufuatiliaji wa hali ya mazingira kwa wakati halisi kupitia teknolojia za kisasa.
Mapema, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Masauni alisema Serikali ipo katika hatua za mwisho za kufanya maboresho ya kisheria yatakayoiwezesha NEMC kuwa na nguvu zaidi katika usimamizi wa sheria za mazingira pamoja na uwezo wa kujitegemea kifedha katika utekelezaji wa majukumu yake.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), Elizabeth Mrema alisema Tanzania imeendelea kuwa mfano mzuri katika usimamizi wa mazingira barani Afrika kupitia ushirikiano wa kimataifa, sera na mifumo ya utekelezaji wa mazingira.
“Tanzania ina miradi ya uhifadhi mazingira yenye thamani ya dola za Marekani milioni 54 na kuifanya kuwa nchi ya kwanza barani Afrika na ya nne duniani kwa kupata ufadhili.”
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Semesi alisema maadhimisho ya miaka 40 ya taasisi hiyo ni fursa ya kutafakari mafanikio yaliyopatikana katika usimamizi wa mazingira nchini pamoja na kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto mpya za mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.






No comments:
Post a Comment