WIZARA YA ARDHI YASIKILIZA MASHAURI 23,426 YA ARDHI, MABARAZA MAPYA SITA YAANZISHWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, May 28, 2026

WIZARA YA ARDHI YASIKILIZA MASHAURI 23,426 YA ARDHI, MABARAZA MAPYA SITA YAANZISHWA


Na Okuly Julius,OKULY BLOG,DODOMA


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo amesema Wizara imeendelea kuimarisha utoaji wa haki katika sekta ya ardhi kwa kusikiliza mashauri 23,426 kupitia Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya pamoja na kuanzisha Mabaraza mapya sita katika mwaka wa fedha 2025/2026.

Dkt. Akwilapo amesema hayo bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Amesema kati ya mashauri yote yaliyosikilizwa hadi Mei 15, 2026, jumla ya mashauri 12,644 yameshughulikiwa na kutolewa uamuzi huku mashauri 10,782 yakiendelea kushughulikiwa.

“Wizara imeendelea kusimamia na kuanzisha Mabaraza mapya katika wilaya mbalimbali nchini ambayo yamekuwa yakisikiliza na kuamua mashauri ya ardhi kwa lengo la kuwapatia wananchi haki kwa wakati,” amesema Dkt. Akwilapo.

Ameeleza kuwa katika mwaka 2025/2026, Wizara ilipanga kuanzisha Mabaraza mapya 24 pamoja na kushughulikia mashauri ya ardhi 16,000, huku hadi sasa Mabaraza sita mapya tayari yameanzishwa na kufanya jumla ya Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya yanayofanya kazi nchini kufikia 121.

Kwa mwaka wa fedha 2026/2027, amesema Wizara imepanga kuanzisha Mabaraza mapya 18 ili kufikia lengo la kuwa na Mabaraza ya Ardhi na Nyumba katika wilaya zote 139 zilizopo nchini.

Aidha, amesema Wizara itaendelea kushughulikia mashauri 10,782 yaliyobaki pamoja na mashauri mapya yatakayofunguliwa ili kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati.

Dkt. Akwilapo pia ametoa wito kwa wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya kuzingatia weledi, uadilifu na misingi ya utoaji haki katika kuamua mashauri ya ardhi ili kuimarisha imani ya wananchi kwa vyombo hivyo vya utoaji haki.

No comments:

Post a Comment