Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imetangaza vipaumbele nane itakavyovitekeleza katika mwaka wa fedha 2026/2027 kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa ardhi, kuboresha huduma kwa wananchi na kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo amesema Serikali itaongeza kasi ya upangaji, upimaji, umilikishaji na usajili wa ardhi mijini, vijijini pamoja na maeneo ya kimkakati.
Amesema Wizara pia imepanga kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji ili kuhakikisha matumizi bora ya ardhi na kupunguza migogoro inayotokana na matumizi holela ya maeneo mbalimbali.
Katika kuboresha utoaji wa huduma, Dkt. Akwilapo amesema Wizara itaendelea kuimarisha mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utunzaji wa kumbukumbu, ukusanyaji wa maduhuli, utoaji wa huduma pamoja na upatikanaji wa taarifa za ardhi na uthamini.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro ya ardhi kupitia Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya ili kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati.
Kwa upande wa makazi, Waziri huyo amesema Wizara itahakikisha uwepo wa nyumba bora pamoja na kukuza sekta ya milki na maendeleo ya makazi kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Amesema vipaumbele vingine ni pamoja na kuimarisha mipaka ya kimataifa na kuendeleza miji ya mipakani, kuongeza upatikanaji wa ramani kwa ajili ya mipango ya kitaifa pamoja na kuimarisha mifumo ya usimamizi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa vipaumbele vya Wizara.
Dkt. Akwilapo amesema utekelezaji wa vipaumbele hivyo utaisaidia Serikali kuongeza ufanisi katika usimamizi wa ardhi na utoaji wa huduma kwa wananchi nchini kote.


No comments:
Post a Comment