NACTVET YAFUNGUA UDAHILI , WAOMBAJI WATAKIWA KULINDA TAARIFA ZAO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, May 28, 2026

NACTVET YAFUNGUA UDAHILI , WAOMBAJI WATAKIWA KULINDA TAARIFA ZAO



Na Okuly Julius, OKULY BLOG , DODOMA


BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), limetangaza rasmi kufunguliwa kwa dirisha la kudahili wanafunzi kwa ngazi ya Astashahada na Stashahada kwa mwaka wa masomo 2026/2027, huku likiwataka waombaji kuwa waangalifu na kulinda taarifa zao za siri.

Udahili huo unahusisha kozi zote zinazosimamiwa na baraza hilo ambapo awamu ya kwanza imeanza rasmi leo Mei 28 na itafikia kikomo Julai 10, 2026.

Akizungumza jijini Dodoma, Mei 28,2026 wakati wa kutoa Taarifa kwa Umma, Katibu Mtendaji wa NACTVET, Dkt. Mwajuma Lingwanda amesema kuwa baraza limejipanga kikamilifu kuhakikisha mchakato huo unakuwa wa uwazi na unatoa fursa sawa kwa kila mwananchi mwenye sifa stahiki.

Dkt. Lingwanda amebainisha kuwa, ili kurahisisha utaratibu huo, mifumo miwili itatumika kulingana na aina ya kozi na maeneo kijiografia.

“Maombi ya kozi za Afya na Sayansi Shirikishi kwa upande wa Tanzania Bara yatafanyika kidijitali kupitia Mfumo wa Udahili wa Pamoja (Central Admission System - CAS) unaopatikana kwenye tovuti yetu rasmi ya www.nactvet.go.tz,” amesema Dkt. Lingwanda.

Kuhusu maombi ya kozi zisizo za afya nchi nzima, pamoja na kozi za Afya na Sayansi Shirikishi kwa vyuo vilivyopo Zanzibar, Katibu Mtendaji huyo amefafanua kuwa waombaji wanapaswa kutuma maombi yao moja kwa moja kwenye vyuo husika kuanzia leo hadi Julai 10, 2026.

Katika hatua nyingine, Dkt. Lingwanda ametoa onyo kali kwa waombaji dhidi ya watu wanaoweza kuwatapeli au kuwasumbua wakati wa mchakato huo, akiwataka kufanya maombi hayo wao wenyewe kwa umakini mkubwa.

“Baraza linasisitiza kila mwombaji kuhusika mwenyewe katika zoezi zima la kuomba kudahiliwa. Ni muhimu kuandika taarifa kwa usahihi na umakini, na kubwa zaidi, kutunza kumbukumbu na namba za simu walizojisajilia bila kumshirikisha mtu mwingine ili kuepuka usumbufu,” amesisitiza.

Ameongeza kuwa, mwanafunzi atakayechaguliwa atatumiwa ujumbe mfupi wa simu (SMS) kutoka NACTVET ukiwa na msimbo (code) maalum wa siri ambao atatakiwa kuuwasilisha chuoni siku ya kuripoti. Baada ya kusajiliwa, wanafunzi wanapaswa kuingia tena kwenye tovuti ya baraza kufanya uhakiki wa taarifa zao kupitia sehemu ya 'Student’s information verification'.

Amesema ili kuondoa mkanganyiko wa maombi, kiongozi huyo ameshauri jamii na waombaji kupakua Kitabu cha Mwongozo wa Udahili (Admission Guidebook for Academic Year 2026/2027) kilichopo kwenye tovuti yao, ambacho kina orodha kamili ya vyuo vyote vilivyosajiliwa na kozi wanazotoa.

Hata hivyo, amevitaka vyuo vyote nchini kuzingatia kikamilifu sheria, kanuni, na miongozo ya baraza wakati wote wa mchakato huo wa kudahili wanafunzi wapya ili kulinda ubora wa elimu ya ufundi nchini.


No comments:

Post a Comment