
Kaimu Mtendaji Mkuu wa UCSAF,Mhandisi Albert Richard wakati akitoa wasilisho katika mafunzo ya wahariri wa vyombo vya habari Mkoa wa Dodoma yaliyofanyika Mei 15, 2026.
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, Dodoma
Jumla ya walimu 3,808 wa shule za msingi na sekondari pamoja na wanafunzi wa kike 1,300 kutoka shule za umma nchini wamenufaika na mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yanayotolewa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kupitia programu mbalimbali zinazolenga kuimarisha matumizi ya teknolojia katika sekta ya elimu.
Hayo yameelezwa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa UCSAF,Mhandisi Albert Richard wakati akitoa wasilisho katika mafunzo ya wahariri wa vyombo vya habari Mkoa wa Dodoma yaliyofanyika Mei 15, 2026.
Mhandisi Richard amesema tangu mwaka wa fedha 2016/2017, UCSAF imeendelea kugharamia mafunzo ya TEHAMA kwa walimu wa shule za msingi na sekondari za umma Tanzania Bara na Zanzibar kwa lengo la kuwaongezea uwezo wa kutumia teknolojia katika ufundishaji na ujifunzaji.

Amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026 pekee, walimu 606 wamepatiwa mafunzo hayo, wakiwemo walimu 100 kutoka Zanzibar na walimu 506 kutoka Tanzania Bara.
“Lengo la mafunzo haya ni kuwawezesha walimu kutumia vifaa vya TEHAMA kwa ufanisi pamoja na kutatua changamoto zinazohusiana na matumizi ya teknolojia katika mazingira ya shule,” amesema Mhandisi Richard.
Aidha, amesema UCSAF imeendelea kuwainua wasichana katika sekta ya teknolojia kupitia maadhimisho ya Girls in ICT Day, ambapo wanafunzi hupatiwa mafunzo ya matumizi ya TEHAMA, ubunifu wa kidijitali pamoja na fursa mbalimbali zinazopatikana katika sekta hiyo.
Kwa mujibu wa Mhandisi Richard, jumla ya wasichana 1,300 tayari wamenufaika na programu hiyo huku lengo kuu likiwa ni kupunguza pengo la ushiriki kati ya wasichana na wavulana katika masuala ya TEHAMA na kuwahamasisha wasichana kujikita katika masomo ya sayansi na teknolojia.
Ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026, UCSAF kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imefanikiwa kuwapatia mafunzo ya TEHAMA wasichana 440 kutoka shule za msingi, sekondari, vyuo, elimu ya awali pamoja na wenye ulemavu katika vituo vya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya na Zanzibar.
Kwa upande wa baadhi ya walimu wa shule za umma walionufaika na mafunzo ya TEHAMA yaliyoandaliwa na UCSAF katika Chuo Kikuu cha Dodoma kuanzia Januari 5 hadi 9, wamesema mafunzo hayo yataongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku shuleni.

Mwl. Cletus Alex amesema elimu waliyoipata itawasaidia kutumia teknolojia katika ufundishaji na kurahisisha utoaji wa maarifa kwa wanafunzi kupitia matumizi sahihi ya vifaa vya TEHAMA.

Kwa upande wake, Mwl. Andrew Mpunje, kutoka Sekondari ya Mount Samba, iliyopo Wilaya ya Kibondo Mkoani Kigoma, amesema kabla ya mafunzo hayo walikuwa wanakutana na changamoto mbalimbali kutokana na kutokuwa na uelewa wa matumizi sahihi ya kompyuta, hali iliyokuwa ikikwamisha baadhi ya shughuli za kitaaluma na kiutendaji shuleni.

Naye Mwl. Pascallina Paul amesema maarifa waliyojifunza watakwenda kuyatumia kwa vitendo katika shule zao kwa kuwafundisha wanafunzi pamoja na walimu wenzao matumizi bora ya TEHAMA ili kuongeza ufanisi katika sekta ya elimu.
Mhandisi Richard amesisitiza kuwa UCSAF itaendelea kuwekeza katika elimu ya kidijitali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha walimu, wanafunzi na vijana kwa ujumla wanapata ujuzi wa teknolojia unaowawezesha kuendana na kasi ya maendeleo ya dunia ya kidijitali.
Amesema uwekezaji huo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kujenga jamii yenye maarifa ya TEHAMA, kuongeza ubunifu kwa vijana na kuandaa nguvu kazi yenye ushindani katika uchumi wa kisasa unaotegemea teknolojia.






No comments:
Post a Comment