Na Mwandishi Wetu - Dodoma.
Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Dodoma, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Crister Kayombo, amewataka wanaume wanaofanyiwa vitendo vya ukatili na wenza wao kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi na kuachana na dhana ya kufumbia macho vitendo hivyo kwa kuogopa kuchekwa na jamii inayowazunguka.
ASP Kayombo amesema hayo Mei 28, 2026 alipokuwa akizungumza katika kikao cha walimu na watoa huduma wa Shule ya Msingi Elishadai jijini Dodoma, ambapo alieleza kuwa baadhi ya wanaume wamekuwa wakipigwa na wenza wao lakini hushindwa kuripoti katika mamlaka husika ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
Aidha, ASP Kayombo alieleza aina mbalimbali za ukatili pamoja na vitendo vya ukatili vinavyoweza kutokea shuleni, ikiwemo ukatili wa kimwili unaotokana na utoaji wa adhabu kinyume na sheria kwa wanafunzi na kusababisha madhara.
Alisema kuwa kuna miongozo maalum ya utoaji adhabu kwa wanafunzi, hivyo mwalimu au mlezi anayetoa adhabu kupita kiasi na kusababisha madhara anaweza kuchukuliwa hatua za kisheria.
Vilevile, ASP Kayombo amesema vitendo vya ukatili dhidi ya wanafunzi vinaathiri maendeleo yao kitaaluma, hivyo walimu wanapaswa kuweka mazingira rafiki yatakayowezesha wanafunzi kutoa taarifa sahihi kuhusu viashiria vya ukatili wanavyokumbana navyo.
“Niwapongeze walimu kwa kuwa mabalozi wazuri wa kugundua vitendo vya ukatili dhidi ya watoto kuliko hata baadhi ya wazazi na walezi ambao hukaa na watoto muda mwingi majumbani bila kubaini viashiria vya ukatili walionavyo, hususan vitendo vya ulawiti na mimba za utotoni,” alisema ASP Kayombo.
Pia amewaasa walimu na walezi kufuatilia kwa karibu malezi na makuzi ya watoto pamoja na kudhibiti maeneo yanayoweza kuchochea vitendo vya ukatili shuleni, ikiwemo vyooni na katika vyumba vya mapumziko.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shule ya Elishadai, Juliana Kallinga, amesema licha ya shule hiyo kufanya vizuri kitaaluma katika ngazi mbalimbali, pia imewekeza katika malezi bora kwa watoto.
Amepongeza Jeshi la Polisi kwa kutembelea shule hiyo na kutoa elimu kwa walimu na walezi, akisema elimu hiyo itasaidia kuleta mabadiliko chanya katika jamii.






No comments:
Post a Comment