WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA UINGEREZA TANZANIA. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, May 22, 2026

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA UINGEREZA TANZANIA.


Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt Rhimo Nyansaho, tarehe 20, Mei, 2026 amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Mheshimiwa Marianne Young aliyemtembelea Waziri wa Ulinzi na JKT katika Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa, Kikombo jijini Dodoma.

Balozi Marianne Young,alifika Wizara ya Ulinzi kuonana na Waziri wa Ulinzi na JKT Dkt Rhimo Nyansaho kwa ajili ya kujitambulisha na kufanya mazungumzo na Waziri Nyansaho kwa lengo la kuendelea kuimarisha uhusiano wa miaka mingi wa maeneo ya ushirikiano kati ya Wizara ya Ulinzi na JKT na serikali ya Uingereza katika masuala ya Ulinzi na Usalama wa kimataifa, mafunzo na vita dhidi ya Ugaidi na usalama wa majini.

Balozi Young alimueleza Waziri wa Ulinzi na JKT utayari wa nchi ya Uingereza kushirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali yanayohusiana na Wizara ya Ulinzi na nchi kwa ujumla.

Balozi Marianne Young alimwambia Waziri Nyansaho, kuwa Tanzania ni nchi muhimu kwa Uingereza kutokana na uhusiano wa muda mrefu na wa kihistoria wa nchi hizi mbili, na ingependa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali za Kiuchumi, Utamaduni na Kijamii.

Balozi Marianne Young akatumia fursa hiyo ya kukutana na Waziri wa Ulinzi na JKT kuipongeza wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kwa kuzindua Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa, Kikombo na kuendelea kuliwezesha Jeshi la Wananchi wa Tanzania kuendelea kutimiza majukumu yake kwa weredi na uzalendo.

Waziri wa Ulinzi Dkt Rhimo Nyansaho, amemshukuru Balozi Marriane Young kwa kutembelea Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa, na kufanya mazungumzo yanayohusu ushirikiano katika sekta ya Ulinzi na Usalama na akatoa rai kwa pande zote mbili kuendelea kushirikiana katika utekelezaji wa makubaliano yaliyopo na kubaini maeneo mapya ya ushirikiano baina ya Tanzania na Uingereza.

Mazungumzo kati ya Waziri wa Ulinzi na JKT na Balozi Marriane Young, yalihudhuriwa na maafisa waandamizi toka Ubalozi wa Uingereza.







No comments:

Post a Comment