Usalama wa maji kwa matumizi ya kijamii na
kiuchumi umepewa kipaumbele kikuu katika mwaka wa fedha 2026/2027, huku
Serikali ikilenga kutumia rasilimali hiyo kama kichocheo cha mageuzi ya uchumi
kwa mujibu wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi
ya Wizara ya Maji, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso,
amesema Wizara imeweka mikakati mahsusi kuhakikisha upatikanaji wa maji unakuwa
wa uhakika na endelevu nchini.
Aweso amesema miongoni mwa vipaumbele vikuu
ni kukamilisha maandalizi ya Mpango Kabambe wa Taifa wa Maji (National Water
Master Plan) ambao utatoa mwongozo wa muda mrefu wa usimamizi, matumizi na
uwekezaji katika rasilimali za maji.
Aidha, amesema Serikali itaendelea na
utekelezaji wa Gridi ya Taifa ya Maji (National Water Grid), unaolenga
kuunganisha vyanzo vikuu vya maji ikiwemo maziwa, mito mikubwa na mabwawa ili
kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama katika maeneo yote
ya nchi.
Katika utekelezaji huo, Wizara imekamilisha
usanifu wa mradi wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Dodoma kupitia
Singida, huku ikiendelea na usanifu wa miradi ya maji kutoka Ziwa Tanganyika na
Ziwa Nyasa, pamoja na mradi wa kutoa maji kutoka Mto Rufiji kupeleka Dar es
Salaam na mkoa wa Pwani.
Kwa upande wa uvunaji wa maji ya mvua, Aweso
amesema Wizara imepanga kujenga na kukarabati mabwawa 33, kufanya usanifu wa
mabwawa mapya 34, pamoja na kuchimba visima virefu 300 katika maeneo yenye
uhaba wa maji.
Katika kuongeza kasi ya upatikanaji wa
huduma, Wizara imepanga kukamilisha miradi 992 ya maji vijijini, miradi 196 ya
maji mijini pamoja na miradi 26 ya usafi wa mazingira, hatua itakayosaidia
wananchi kunufaika kwa wakati na uwekezaji wa Serikali.
Aweso amesema Serikali pia itaanza utekelezaji
wa miradi ya maji katika vijiji 314 ambavyo bado havina huduma, ikiwa ni sehemu
ya mpango wa kufikia vijiji 1,575 ambavyo havijafikiwa na huduma hiyo.
Katika kudhibiti upotevu wa maji, Wizara
itaongeza matumizi ya teknolojia za kisasa ikiwemo mifumo ya usomaji mita kwa
njia ya kielektroniki na ufuatiliaji wa mitandao ya maji, sambamba na kuchukua
hatua za kisheria dhidi ya waharibifu wa miundombinu na wizi wa maji.
Aidha, Wizara imeweka kipaumbele katika
kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira katika vituo vya afya na shule,
kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha huduma hizo muhimu
zinapatikana kwa uhakika na kusaidia kulinda afya za wananchi.
Aweso amesisitiza kuwa utekelezaji wa
vipaumbele hivyo utaenda sambamba na kuimarisha usimamizi wa miradi, matumizi
bora ya fedha za umma na kuhakikisha huduma za maji zinakuwa chachu ya
maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
.jpeg)

No comments:
Post a Comment