WMA YAHAKIKI NA KUKABIDHI MIZANI 5 SOKO KUU LA MAJENGO DODOMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, May 19, 2026

WMA YAHAKIKI NA KUKABIDHI MIZANI 5 SOKO KUU LA MAJENGO DODOMA


Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Wakala wa Vipimo nchini (WMA) umeonya dhidi ya tabia ya kufanya biashara kwa makadirio ukisema matumizi ya makopo, vifurushi na vipimo visivyo rasmi vinachangia hasara kwa wafanyabiashara na unyonyaji kwa wanunuzi, hali inayoweza kudhoofisha kufikiwa kwa uchumi imara.


Akizungumza jijini Dodoma kuelekea maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani yanayoadhimishwa kila Mei 20, Meneja wa (WMA) Mkoa wa Dodoma , Said Ibrahimu, amesema Wakala huo umeendelea kufanya ukaguzi na uhakiki wa vipimo katika masoko, maduka na maghala ili kuhakikisha biashara zinafanyika kwa kuzingatia vipimo sahihi.

Katika kuhamasisha matumizi ya mizani sahihi, WMA imekagua na kukabidhi mizani mitano kwa wafanyabiashara wa Soko Kuu la Majengo ikiwa ni sehemu ya kampeni ya utoaji elimu kwa wafanyabiashara na wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi ya vipimo sahihi.

Said amesema haiwezekani kufikia uchumi imara ikiwa bado kuna watu wanaouza bidhaa kwa kutumia makopo au vifurushi badala ya mizani iliyohakikiwa rasmi na Serikali.

Amesema WMA itaendelea kufanya ukaguzi wa kushtukiza katika maeneo mbalimbali ya biashara ili kubaini watu wanaochezea mizani au kutumia vipimo visivyo sahihi, huku hatua za kisheria zikichukuliwa dhidi ya watakaobainika kukiuka sheria.

“Biashara inayofanyika kwa kukadiria inaweza kumsababishia mfanyabiashara hasara au kumnyonya mnunuzi, hivyo tunaendelea kutoa elimu na kuhamasisha matumizi sahihi ya mizani kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla,” amesema Said.

Aidha, amesema maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani yanapaswa kuwa fursa ya kuwakumbusha wananchi umuhimu wa kutumia vipimo sahihi ili kulinda haki za muuzaji na mnunuzi.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Soko Kuu la Majengo, Fred Grayson, ameishukuru WMA kwa kulichagua soko hilo kuwa sehemu ya kampeni ya kuhamasisha matumizi ya mizani kuelekea maadhimisho hayo.

Naye mfanyabiashara wa soko hilo, Hadija Abdala, amesema matumizi ya mizani ni njia muhimu ya kumwepusha mfanyabiashara na hasara huku akiwataka wanunuzi kudai matumizi ya mizani wanaponunua bidhaa mbalimbali.

No comments:

Post a Comment