Washiriki wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wadau wa Tasnia ya Maziwa mkoani Mbeya wamepata fursa ya kujifunza kwa vitendo kupitia ziara maalum zilizofanyika katika kiwanda cha maziwa cha Chuo Kikuu Cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) pamoja na shamba la ng’ombe wa maziwa la Gereza la Songwe, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uelewa wao kuhusu uzalishaji, uchakataji na usimamizi wa ubora wa maziwa.
Ziara hizo zimefanyika mara baada ya washiriki hao kupata mafunzo ya nadharia kuhusu dhana ya Afya Moja (One Health), usalama wa maziwa, udhibiti wa magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu pamoja na matumizi sahihi ya teknolojia katika mnyororo wa thamani wa maziwa.
Katika kiwanda cha maziwa cha MUST, washiriki walijionea namna maziwa yanavyopokelewa, kuchujwa, kuchemshwa, kupozwa na kufungashwa kwa kutumia mitambo mbalimbali ya kisasa inayotumika kuhakikisha maziwa yanakuwa salama na yenye ubora unaokidhi viwango vinavyotakiwa.
Akitoa maelezo kwa washiriki hao, Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Chakula na Teknolojia kutoka Chuo Kikuu Cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) Dkt. Joseph Runyogote alisema matumizi sahihi ya teknolojia katika uchakataji wa maziwa yana mchango mkubwa katika kuongeza usalama wa maziwa, kuongeza muda wa matumizi ya bidhaa pamoja na kuongeza thamani ya maziwa yanayozalishwa na wafugaji.
Kwa upande wa shamba la ng’ombe wa maziwa la Gereza la Songwe, washiriki walipata fursa ya kujifunza mbinu bora za ufugaji wa kisasa, lishe ya mifugo, usimamizi wa afya za ng’ombe pamoja na namna bora ya uzalishaji wa maziwa kwa kuzingatia usafi na mazingira. Ziara hiyo iliwasaidia washiriki kuona kwa vitendo namna mifumo bora ya ufugaji inavyoweza kuongeza uzalishaji wa maziwa na kuboresha kipato cha wafugaji.
Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo alisema ziara za vitendo zimewaongezea uelewa mkubwa kuhusu uchakataji wa maziwa, matumizi ya teknolojia pamoja na usimamizi wa ubora wa maziwa kuanzia shambani hadi kwa mlaji wa mwisho.
Alieleza kuwa elimu waliyoipata itawasaidia kuboresha shughuli zao za uzalishaji na usambazaji wa maziwa kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu na usalama wa walaji.
Mafunzo hayo yaliyofanyika kwa siku nne katika Ukumbi wa Chuo Kikuu Cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) yakilenga kuwajengea uwezo wadau wa Tasnia ya Maziwa kuhusu usalama wa maziwa, afya ya jamii na matumizi ya teknolojia bora katika kukuza Tasnia ya Maziwa nchini yameendeshwa na Bodi ya Maziwa Tanzania wakishirikiana na Wakala ya Maabara ya Veterinari (TVLA), Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) pamoja Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kwa udhamini wa nchi ya Norway.






No comments:
Post a Comment