WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, amesema kuwa sera ya ulinzi ni mhimili muhimu unaolinda usalama wa taifa na kuweka msingi imara wa maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha uwezo wa taifa wa kukabiliana na changamoto za kiusalama zinazojitokeza katika mazingira ya sasa ya dunia.
Dkt. Nyansaho ametia kauli hiyo Aprili 4, 2026 alipowasilisha mhadhara wa kimkakati katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania (National Defence College – Tanzania) kilichopo Kunduchi, Dar es Salaam, kwa washiriki wa Kozi ya Kistrategia ya 14, chini ya mada "Umuhimu wa Sera ya Ulinzi katika Kuimarisha Usalama wa Taifa."
Katika mhadhara wake, Waziri Nyansaho ameeleza kuwa sera ya ulinzi si nyaraka za kawaida za serikali bali ni dira inayotoa mwongozo wa kimkakati katika kulinda mipaka, watu na rasilimali za taifa, huku ikihakikisha nchi inakuwa salama na yenye utulivu wa kutosha kuendeleza shughuli za maendeleo.
"Usalama wa taifa ni msingi wa maendeleo. Bila usalama, ustawi wa uchumi, uwekezaji na huduma za kijamii haviwezi kufikiwa kwa ufanisi unaotarajiwa," amesisitiza Waziri Nyansaho.
Ameongeza kuwa mabadiliko ya teknolojia, ongezeko la uhalifu wa kimtandao, migogoro ya kikanda na changamoto nyingine za kiusalama zinahitaji sera madhubuti na taasisi imara za ulinzi na usalama zinazoweza kujibu kwa wakati na ufanisi.
Pia Dkt. Nyansaho amesisitiza kuwa mafanikio ya utekelezaji wa sera ya ulinzi yanategemea ushirikiano wa karibu kati ya vyombo vya ulinzi na usalama, taasisi mbalimbali za serikali, sekta binafsi na wananchi kwa ujumla.
"Kulinda usalama wa taifa si jukumu la vyombo vya ulinzi pekee, bali ni wajibu wa kila Mtanzania. Uzalendo, mshikamano na utayari wa kutetea maslahi ya taifa ni nguzo muhimu katika kujenga taifa salama na lenye maendeleo endelevu," amesema.
Awali, Waziri Nyansaho alipokelewa na Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi, Balozi Meja Jenerali Wilbert Ibuge, ambaye alimweleza kuhusu shughuli, majukumu na mafanikio ya chuo hicho katika kuandaa viongozi wa ngazi za juu wenye uwezo wa kuchambua na kusimamia masuala ya ulinzi, usalama na maendeleo ya taifa.
Mhadhara huo ni sehemu ya programu ya mafunzo ya kimkakati inayotolewa na chuo hicho, yenye lengo la kuwajengea washiriki uelewa wa kina kuhusu masuala ya ulinzi na usalama katika mazingira ya kitaifa, kikanda na kimataifa, sambamba na kuandaa viongozi wenye uwezo wa kufanya maamuzi ya kimkakati kwa manufaa ya Taifa.







No comments:
Post a Comment