JAB, UDOM ZAIMARISHA USHIRIKIANO KUBORESHA TAALUMA YA HABARI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, June 5, 2026

JAB, UDOM ZAIMARISHA USHIRIKIANO KUBORESHA TAALUMA YA HABARI


Na Mwandishi Wetu

Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) inaandaa mapendekezo ya kufanya maboresho ya Kanuni za Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, ili kuwezesha wahitimu wa taaluma za Habari, Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma kupata ithibati bila sharti la kuwasilisha barua ya mwajiri.

Hayo yamesemwa leo tarehe 05 Juni, 2026 na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, wakati akiwasilisha mada kuhusu “Uhuru wa Vyombo vya Habari katika Enzi ya Kidijiti: Wajibu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari” kwenye Kongamano la Uhuru wa Vyombo vya Habari lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kupitia Idara ya Sanaa na Taaluma za Habari.

Wakili Kipangula amesema maboresho hayo yanalenga kupanua wigo wa wanufaika wa mfumo wa ithibati kwa kuwajumuisha wahitimu wa taaluma hizo mara tu wanapomaliza masomo yao, hatua itakayowawezesha kuwa tayari kuingia katika soko la ajira au kujihusisha na shughuli za kitaaluma zinazohitaji ithibati wakati wowote.

Amesema kwa sasa Kanuni za Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, zinamtaka mwombaji wa ithibati kuwasilisha nyaraka za kitaaluma pamoja na barua ya utambulisho kutoka kwa mwajiri au chombo cha habari, taasisi au jukwaa analopeleka kazi zake za kitaaluma.

Kwa mujibu wa Kipangula, mapitio ya kanuni hizo yatawezesha kuondoa changamoto zinazowakabili baadhi ya wahitimu wapya ambao wanakidhi sifa za kitaaluma lakini bado hawajapata waajiri au taasisi za kuwapatia barua za utambulisho zinazohitajika katika mchakato wa maombi ya ithibati.

Awali kabla ya kumkaribisha Wakili Kipangula kutoa wasilisho Mkuu wa Idara ya Sanaa na Taaluma za Habari katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dkt. Deograsia Ndunguru, ameikaribisha Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) kuendelea kuimarisha ushirikiano na Chuo hicho katika maeneo mbalimbali, ikiwemo maboresho ya mitaala ya uandishi wa habari ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya sekta ya habari.



No comments:

Post a Comment