Mawaziri wa EAC Waazimia Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, June 4, 2026

Mawaziri wa EAC Waazimia Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji


Mawaziri wenye dhamana ya sekta za Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wameazimia kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuongeza ushindani wa uchumi wa kikanda, kuimarisha mtangamano wa soko la pamoja na kuchochea maendeleo ya viwanda katika Jumuiya.

Azimio hilo limefikiwa katika Mkutano wa 48 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika Juni 4, 2026 katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Arusha.

Mkutano huo ulitanguliwa na kikao cha wataalamu kilichofanyika kuanzia Mei 29 hadi Juni 1, 2026, na baadaye kufuatiwa na kikao cha Makatibu Wakuu kilichofanyika Juni 2 hadi 3, 2026. Vikao hivyo vilijadili masuala mbalimbali kuhusu biashara na uwekezaji kabla ya kuwasilisha mapendekezo kwa mawaziri kwa ajili ya maamuzi.

Katika mkutano huo, mawaziri walipokea, kujadili na kuridhia mapendekezo yaliyowasilishwa na Kamati ya Forodha, Kamati ya Viwango ya Afrika Mashariki, Kamati ya Uwekezaji, Kamati ya Ushindani ya Afrika Mashariki pamoja na Kamati ya Maendeleo ya Viwanda. Mapendekezo hayo yanalenga kuimarisha utekelezaji wa sera na programu zinazolenga kuongeza biashara katika Jumuiya, kuhamasisha uwekezaji na kukuza sekta ya viwanda katika nchi wanachama.

Mawaziri hao pia wameliridhia mapitio ya Kanuni za Uasili wa Bidhaa za Afrika Mashariki (Rules of Origin), hatua inayolenga kulinda soko la bidhaa zinazozalishwa ndani ya Jumuiya pamoja na kuongeza matumizi ya malighafi za ndani, kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vya kuongeza thamani, kuchochea uzalishaji wa bidhaa, kutengezea ajira mpya na kuongeza ushindani wa bidhaa za EAC katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Aidha, mawaziri wamekubaliana kuongeza kasi ya kuondoa vikwazo vya biashara visivyo vya ushuru (NTBs) ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Mkutano wa 25 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya, wakikusudia kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara, kufupisha muda wa usafirishaji wa bidhaa na huduma mipakani na kuimarisha mazingira ya uwekezaji katika Jumuiya.


SCTIFI ni moja ya vyombo muhimu vya kisekta vya EAC vinavyosimamia utekelezaji wa sera na mikakati ya biashara, viwanda, fedha na uwekezaji. Maamuzi yake yana mchango mkubwa katika kuimarisha soko la pamoja la EAC, kuongeza biashara ya ndani ya Jumuiya na kuifanya Afrika Mashariki kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji barani Afrika.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo uliongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. James Millya (Mb), ukijumuisha Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Pius Chaya; Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Kaimu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa; Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Dkt. Habiba Hassan Omar; pamoja na maafisa wengine waandamizi wa Serikali.






No comments:

Post a Comment