Na Okuly Julius, OKULY BLOG, Dodoma
SERIKALI imesema Mpango wa Grand Challenges Tanzania utachochea upatikanaji wa suluhisho bunifu kwa changamoto za maendeleo nchini, huku mafanikio yake yakipimwa kwa namna yatakavyoboresha maisha ya wananchi.
Kauli hiyo imetolewa Mei 4,2026 jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, wakati wa uzinduzi rasmi wa mpango huo kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda.
Amesema mpango huo ni hatua muhimu katika kuimarisha matumizi ya sayansi, teknolojia, utafiti na ubunifu kama nyenzo za kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
“Mpango huu unatoa fursa ya kukuza tafiti na bunifu za ndani, kuimarisha ushirikiano wa wadau na kuhakikisha matokeo ya tafiti yanawanufaisha wananchi moja kwa moja,” amesema.
Ameeeleza kuwa kuchaguliwa kwa Tanzania kuwa mshirika wa Jumuiya ya Grand Challenges ni ishara ya imani kubwa kwa watafiti na taasisi za nchini katika kutafuta suluhisho endelevu za changamoto za maendeleo.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa watafiti na wabunifu ili kuongeza mchango wa sayansi na teknolojia katika maendeleo ya taifa, hususan katika sekta za afya, kilimo na nishati safi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Dkt. Islam Seif Salum, amesema mpango huo unatoa fursa ya kuelekeza maarifa na ubunifu katika kutafuta majawabu ya changamoto za maendeleo zinazohitaji uwekezaji zaidi katika utafiti na teknolojia.
Amesema Zanzibar ina mchango mkubwa katika maeneo ya utafiti na ubunifu, hususan katika uhifadhi wa mazingira ya pwani na bahari, nishati jadidifu na afya ya jamii.
Dkt. Salum amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za utafiti, vyuo vikuu, sekta binafsi na washirika wa maendeleo, akibainisha kuwa mafanikio ya Tanzania yanategemea uwezo wa pande zote za Muungano kushirikiana, kubadilishana maarifa na kutumia ubunifu kwa maendeleo ya wananchi wote.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa , Dkt. Amos Nungu, amesema kupitia Mfuko wa Taifa wa Kuendeleza Sayansi na Teknolojia (NFAST), zaidi ya Sh bilioni 129 zimehamasishwa kusaidia tafiti, ubunifu, maendeleo ya teknolojia na miundombinu ya kisayansi, huku Serikali ikichangia zaidi ya Sh bilioni 85.
Amesema uwekezaji huo umewezesha kuboreshwa kwa maabara, kuimarisha uwezo wa watafiti, kupanua vituo vya ubunifu na kuwapa vijana fursa za ufadhili na mafunzo.
Dkt. Nungu amesema hatua inayofuata ni kuhakikisha matokeo ya tafiti na ubunifu yanageuzwa kuwa sera, teknolojia na huduma zenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi, sambamba na kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu ya taifa.










No comments:
Post a Comment