
Na Boniphace John, Dodoma
KUELEKEA Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imezindua bustani yenye miti 500 katika eneo la Nkuhungu Swai jijini Dodoma na kuwataka Watanzania kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa mazingira kwa kuzingatia falsafa ya 4R inayojumuisha Ustahimilivu, Maridhiano, Mageuzi na Kujenga Upya.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Haki za Binadamu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Nkasori Sarakikya, alisema utunzaji wa mazingira ni sehemu muhimu ya kulinda na kuendeleza haki za binadamu.
Alisema Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu kupitia Kifungu cha 24 unatambua haki ya kila mtu kuishi katika mazingira yanayoridhisha na yanayofaa kwa maendeleo yake.
Aidha, alisema Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kihistoria linalotambua mazingira safi, salama na endelevu kuwa haki ya msingi ya binadamu.
Sarakikya aliongeza kuwa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR), kupitia Maoni ya Jumla Na. 36, unaeleza kuwa uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi ni vitisho vya moja kwa moja kwa haki ya kuishi ya binadamu.
Alisema Serikali inaendelea kusimamia shughuli za uhifadhi na usimamizi wa mazingira kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021 pamoja na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura ya 191, sambamba na kutekeleza wajibu wake katika mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda kuhusu mazingira.
“Mazingira bora hutoa huduma muhimu kwa binadamu kama maji safi, hewa, chakula, dawa, ardhi yenye rutuba na udhibiti wa hali ya hewa. Huduma hizi hutegemea mifumo imara ya ikolojia na uwepo wa bioanuwai,” alisema.
Alibainisha kuwa uharibifu wa mazingira na upotevu wa bioanuwai hupunguza uwezo wa wananchi kufurahia haki zao za msingi, huku akisisitiza kuwa miti ni rasilimali muhimu inayochangia afya na ustawi wa jamii.
Kwa mujibu wa Sarakikya, tafiti mbalimbali zimeonyesha kuwa mazingira ya asili yana mchango mkubwa katika kuboresha afya ya akili kwa kupunguza msongo wa mawazo, kurekebisha mapigo ya moyo, kushusha shinikizo la damu na kuimarisha afya kwa ujumla.
“Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) ya mwaka 2022, hata kuangalia mandhari ya asili kupitia dirishani kunaweza kusaidia kuharakisha uponaji wa majeraha yanayotokana na upasuaji,” alisema.
Kwa upande wao, viongozi wa Serikali ya Mtaa wa Salama Nkuhungu na Chama Cha Mapinduzi (CCM), akiwemo Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, Habas Mwijuki, Katibu wa CCM Kata ya Nkuhungu, Mariam Farijala pamoja na Diwani wa Kata hiyo, waliwahimiza wananchi kupanda na kutunza miti katika maeneo yao ili kuunga mkono juhudi za kujenga Tanzania ya kijani.
Uzinduzi huo uliambatana na kambi ya msaada wa kisheria kwa wananchi wenye malalamiko ya ukiukwaji wa haki za binadamu, usafi wa mazingira na upandaji wa miti 30 iliyoongeza idadi ya miti katika bustani hiyo kutoka 470 hadi kufikia 500.
Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka huu ni “Dira 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania,” ikihimiza Watanzania kuchukua hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhifadhi mazingira kwa maendeleo endelevu.












No comments:
Post a Comment