Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuchukua hatua za haraka kushughulikia mapungufu yaliyoainishwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2025.
Maelekezo hayo yalitolewa katika kikao cha kamati hiyo kilichofanyika Bungeni jijini Dodoma chini ya Mwenyekiti wake, Devota Minja, ambapo wajumbe walisisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya ukaguzi wa ndani, uhakiki wa walipakodi na ufuatiliaji wa mapato ya serikali ili kuzuia upotevu wa fedha za umma.
Akizungumza mbele ya kamati hiyo, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, alisema mamlaka hiyo imepokea maelekezo yote yaliyotolewa na itayafanyia kazi kwa wakati ili kuboresha utendaji wake.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TRA, Uledi Mussa, alisema kikao hicho kimekuwa fursa muhimu ya kutathmini utendaji wa mamlaka hiyo na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho kwa lengo la kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.
TRA imeahidi kuendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kukuza uaminifu kwa walipakodi na kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari, hatua inayolenga kuongeza mapato ya serikali kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.





No comments:
Post a Comment