
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema matumizi ya teknolojia ya kidijitali katika sekta ya sheria yana mchango mkubwa katika kuongeza ufanisi, uwazi na upatikanaji wa huduma za haki kwa wananchi, hususan walioko maeneo ya mbali.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 07 Juni, 2026 alipofungua Mkutano Mkuu wa 26 wa Chama Cha Mawakili Zanzibar(ZLS) uliofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip Airport, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya kidijitali katika Mahakama, ikiwemo mfumo wa e-filing, ufuatiliaji wa mashauri kwa njia ya mtandao na mifumo ya kisasa ya usimamizi wa kesi ili kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wakati.
Aidha, amesisitiza kuwa pamoja na umuhimu wa teknolojia, maadili, uadilifu na uwajibikaji wa watendaji wa sekta ya sheria ni nguzo muhimu katika kuimarisha mfumo wa utoaji haki.
Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi amewahimiza mawakili kuendelea kutoa huduma za kitaaluma kwa uadilifu, kushiriki katika maboresho ya sheria na kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi wasiokuwa na uwezo.
Katika hafla hiyo, Rais Dkt. Mwinyi alipokea Tuzo ya Kiongozi Bora kwa kutambua mchango wake katika uongozi, maendeleo ya jamii na kuimarisha utawala bora.









No comments:
Post a Comment