Rais wa Jamhuri ya Singapore, Mheshimiwa Tharman Shanmugaratnam, ametoa rai kwa nchi za Afrika kubadili changamoto za kimataifa kuwa fursa kwa kuwekeza katika elimu, ukuzaji wa ujuzi, ubunifu, uundaji wa ajira na taasisi imara.
Mheshimiwa Tharman amesema hayo alipozungumza kwenye mhadhara uliofanyika Juni 9,2026 katika Ukumbi wa Maktaba wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo alisema kuwa ukuaji shirikishi ni muhimu ili kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi yanawanufaisha wananchi wote.
Alisisitiza kuwa elimu, afya, teknolojia na kujifunza kwa maisha yote ni nyenzo muhimu ya kuandaa nguvu kazi yenye uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya haraka yanayosababishwa na maendeleo ya teknolojia, Akili Mnemba (AI) na mabadiliko ya tabianchi.
Alieleza kuwa licha ya Afrika kukabiliwa na changamoto hizo, bara hilo lina fursa kubwa kutokana na idadi kubwa ya vijana, rasilimali nyingi za asili na uwezo wa kukuza masoko yake na waafrika hawana budi kugeuza changamoto hizo kuwa fursa kwa ukuaji wa uchumi.
Pia alieleza umuhimu wa kuwekeza katika nishati jadidifu, mafunzo ya ufundi stadi, ushirikiano wa kikanda kupitia Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.
Alisisitiza kuwa utawala bora, uwazi na taasisi madhubuti ni msingi wa maendeleo jumuishi, na kihimiza nchi za Afrika kutumia nguvu, ubunifu na ari ya vijana wake kujenga mustakabali wenye ustawi na fursa kwa wote.







No comments:
Post a Comment