
Na Okuly Julius, OKULY BLOG , DODOMA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, ameagiza mamlaka za nidhamu kuchukua hatua za haraka dhidi ya watumishi wa umma waliobainika kughushi barua za uhamisho pamoja na wote waliohusika katika vitendo hivyo, akisisitiza kuwa Serikali haitavumilia ukiukwaji wa maadili na sheria za utumishi wa umma.
Kikwete ametoa kauli hiyo Juni 1, 2026 jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha siku tatu cha Wakuu wa Idara na Vitengo vya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kutoka Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Amesema Serikali imeendelea kupokea malalamiko kuhusu vitendo vya udanganyifu wa nyaraka, ikiwemo kughushi barua za uhamisho na ajira, hali inayokiuka maadili ya utumishi wa umma na kuathiri ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi.
Kikwete amesema tayari Serikali imeanza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watumishi wanaohusika na vitendo hivyo, huku baadhi yao wakifikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo amewataka waajiri kutokuwa chanzo cha ucheleweshaji wa malipo ya mafao kwa watumishi waliostaafu kwa kushindwa kutekeleza kwa wakati majukumu yao ya kushughulikia madai ya stahiki za wastaafu.
Amesema Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imekuwa ikipokea maombi mengi kutoka kwa wastaafu yanayohusu kucheleweshwa kwa mafao na stahiki mbalimbali ambazo zilipaswa kushughulikiwa katika taasisi wanazotoka.
"Waajiri wanapaswa kutimiza wajibu wao kwa wakati ili kuondoa usumbufu usio wa lazima kwa watumishi waliolitumikia Taifa kwa muda mrefu," amesema.
Aidha, Kikwete amewasisitiza wataalamu wa rasilimaliwatu kuongeza matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika usimamizi wa utumishi wa umma ili kuboresha uwazi, uwajibikaji na kasi ya utoaji huduma kwa wananchi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi, amesema bado kuna changamoto ya ucheleweshaji wa utoaji huduma kwa wananchi katika baadhi ya taasisi za umma kutokana na watumishi kutofuata taratibu, sheria na miongozo ya kiutendaji.
Mkomi amesema watumishi wa umma wanapaswa kuzingatia kikamilifu misingi ya utawala bora, uwajibikaji na weledi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati na kwa ubora unaostahili.
Ameongeza kuwa kikao hicho kinatoa fursa kwa wataalamu wa rasilimaliwatu kujadili changamoto mbalimbali zinazokabili utumishi wa umma na kuweka mikakati ya kuimarisha utoaji wa huduma kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kikao hicho kimewakutanisha Wakuu wa Idara na Vitengo vya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kutoka taasisi mbalimbali za umma nchini kwa lengo la kujadili masuala ya kiutumishi, matumizi ya mifumo ya kidijitali na mbinu za kuboresha utendaji kazi katika sekta ya umma.








No comments:
Post a Comment