SERIKALI YATATUA KERO YA UMEME KONGWA, YAWEKEZA SH. BILIONI 10 KUIMARISHA HUDUMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, June 16, 2026

SERIKALI YATATUA KERO YA UMEME KONGWA, YAWEKEZA SH. BILIONI 10 KUIMARISHA HUDUMA




Na Okuly Julius, OKULY BLOG ,Kongwa


SERIKALI imezindua Kituo cha Kubadilishia Njia za Usambazaji Umeme (Switching Station) pamoja na transfoma mpya katika eneo la Mbande, Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, hatua inayotarajiwa kuondoa kwa kiasi kikubwa changamoto za kukatika kwa umeme na kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo.

Akizindua mradi huo leo, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, alisema uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan za kuimarisha miundombinu ya nishati na kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika kwa matumizi ya nyumbani na shughuli za uzalishaji.

Alisema kwa muda mrefu Wilaya ya Kongwa na maeneo jirani yalikuwa yakikumbwa na changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara kutokana na kutegemea njia moja ya usambazaji, hali iliyosababisha wilaya nzima kuathirika pindi hitilafu ilipotokea katika sehemu yoyote ya mtandao.

“Kwa muda mrefu changamoto ya voltage ndogo na kukatika kwa umeme mara kwa mara ilikuwa kikwazo kikubwa kwa wananchi na wajasiriamali, hususan wanaojishughulisha na shughuli za uzalishaji kama kusaga nafaka na kukamua mafuta. Mradi huu unakwenda kubadili hali hiyo,” alisema Ndejembi.

Alisema zaidi ya Sh bilioni 10 zimewekezwa katika ujenzi wa kituo hicho cha Switching Station na miundombinu yake, uwekezaji ambao utanufaisha wakazi wa Kongwa, Kiteto, Gairo, Chamwino na Mpwapwa kwa kupata huduma ya umeme wa uhakika na wa kutosha.

Ndejembi alisisitiza kuwa dhamira ya Serikali si kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa kuwasha taa pekee, bali umeme wa kuendesha viwanda, biashara na shughuli nyingine za uzalishaji zitakazochochea ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Subira Mgalu, alisema utekelezaji wa miradi ya umeme unaendelea kuleta matokeo chanya kwa wananchi na kuunga mkono jitihada za Serikali za kuharakisha maendeleo ya kiuchumi.

“Tunaona matokeo ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kupitia TANESCO. Changamoto za kukatika kwa umeme zilizokuwa zikisumbua wananchi wa maeneo haya zimepungua kwa kiwango kikubwa,” alisema Mgalu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mayeka Simon Mayeka, aliwataka wananchi na wawekezaji kutumia fursa ya upatikanaji wa umeme wa uhakika kuanzisha viwanda vya usindikaji, biashara na miradi mingine ya kiuchumi itakayochangia maendeleo ya wilaya hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, alisema kabla ya utekelezaji wa mradi huo, wananchi wa Kongwa na maeneo jirani walitegemea njia moja ya umeme ya kilovoti 33 kutoka Dodoma Mjini, hali iliyokuwa ikisababisha changamoto katika utoaji wa huduma kutokana na ongezeko la mahitaji.

“Awali kulikuwa na njia moja ya kusambaza umeme inayopita katika wilaya tano. Kadri mahitaji yalivyoongezeka, changamoto za utoaji wa huduma ziliongezeka pia. Tangu miradi hii ilipoanza kufanya kazi, changamoto hizo zimepungua kwa zaidi ya asilimia 90,” alisema Twange.

Kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika, kuongeza fursa za uwekezaji, kukuza shughuli za kiuchumi na kuboresha utoaji wa huduma za kijamii katika wilaya za Kongwa, Kiteto, Gairo, Chamwino na Mpwapwa.






No comments:

Post a Comment