
Na Okuly Julius, OKULY BLOG , DODOMA
Serikali imeendelea kuimarisha juhudi za kuboresha ubora wa elimu nchini kwa kuhamasisha ubunifu na umahiri wa walimu, huku walimu 3,153 wakijisajili kushiriki Shindano la Taifa la Stadi za Ufundishaji la mwaka 2026 linalolenga kuibua mbinu bora za ufundishaji na kujifunzia.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Afidhi Ameir amesema shindano hilo ni sehemu ya utekelezaji wa mageuzi ya sekta ya elimu pamoja na Mpango Mkakati wa Kisayansi wa Kujenga Umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa watoto wa elimu ya awali na wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuelekea hafla ya utoaji wa zawadi kwa washindi wa Shindano la Taifa la Nne la Stadi za Ufundishaji kwa Walimu wa Shule za Awali na Msingi pamoja na Shindano la Pili kwa Walimu wa Shule za Sekondari Tanzania Bara, amesema serikali inaona shindano hilo kama nyenzo muhimu ya kuongeza ubunifu katika ufundishaji.
“Shindano hili linatoa fursa kwa walimu kuonesha umahiri wao, kubadilishana uzoefu na kuibua mbinu bunifu zinazoweza kusaidia kuongeza ubora wa elimu na matokeo ya ujifunzaji kwa wanafunzi,” amesema.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, kati ya walimu 3,153 waliojisitiri kupitia Mfumo wa Kielektroniki wa National Teaching Skills Competition System (TSCS), walimu 1,263 walikamilisha masharti yote kwa kuwasilisha video za ufundishaji na maandalio ya masomo kwa ajili ya tathmini.
Amesema shindano la mwaka huu limehusisha maeneo saba ya ushindani ambayo ni Kusoma kwa Darasa la Awali, Kiingereza kwa Darasa la Kwanza, Ufaraguzi wa Zana kwa Darasa la Pili pamoja na masomo ya Fizikia, Hisabati, Business Studies na Computer Science kwa walimu wa shule za sekondari.
Ameeleza kuwa maeneo hayo yamechaguliwa kutokana na mchango wake katika kuimarisha stadi za msingi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK), stadi za lugha ya Kiingereza, ujasiriamali pamoja na stadi za karne ya 21.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo amewataka walimu kote nchini kufuatilia mashindano hayo na kujifunza kutoka kwa washiriki waliobobea ili kuongeza ufanisi katika ufundishaji na ujifunzaji darasani.
Aidha, amesema shindano hilo linaunga mkono juhudi za serikali za kutekeleza Mpango Mkakati wa Kisayansi wa Kujenga Umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu uliozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Januari 29, 2026, unaolenga kuhakikisha kila mwanafunzi anapata stadi za msingi kwa kiwango stahiki.
Hafla ya utoaji wa zawadi kwa washindi itafanyika Juni 6, 2026 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Riziki Shemdoe.
Washindi wa nafasi ya kwanza katika kila eneo la ushindani watapata Sh milioni 2.5, kompyuta mpakato, vyeti vya ushindi na pongezi, huku shule zao zikikabidhiwa projekta. Kwa baadhi ya maeneo ya elimu ya awali na msingi, shule za washindi pia zitapatiwa vibao vya kielektroniki 100 vyenye thamani ya Sh milioni tano kwa ajili ya kuimarisha ujifunzaji wa kidijitali.
Kaulimbiu ya shindano la mwaka huu ni “UFUNDISHAJI BORA, TAIFA IMARA.”









No comments:
Post a Comment