TANNA YALAANI SHAMBULIZI LA DAKTARI KWA MUUGUZI, YATAKA HAKI ITENDEKE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, June 14, 2026

TANNA YALAANI SHAMBULIZI LA DAKTARI KWA MUUGUZI, YATAKA HAKI ITENDEKE


Na Boniphace John, Dodoma


Chama cha Wauguzi Tanzania (TANNA) kimelaani vikali tukio la daktari kumshambulia muuguzi akiwa kazini katika Hospitali ya Mji wa Bariadi, Mkoa wa Simiyu, na kutoa wito kwa viongozi wote wenye dhamana kusimamia taaluma, sheria, kanuni na taratibu za kiutumishi kwa haki, usawa na bila upendeleo.

Tukio hilo lilitokea Mei 26, 2026, na TANNA ilipokea taarifa zake siku iliyofuata, Mei 27, ambapo ilianza kufuatilia kwa karibu mwenendo wa suala hilo kwa kushirikiana na viongozi wa tawi la Simiyu pamoja na mamlaka husika.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Rais wa TANNA, Dkt. Ezekiel Mbao, alisema uongozi unaozingatia sheria na kuwajibika kwa wakati ni msingi muhimu wa kujenga mazingira salama ya kazi, kuimarisha mahusiano ya kitaaluma na kudumisha imani ya wananchi kwa mfumo wa huduma za afya.

Alisema chama hicho kimekuwa kikifuatilia kwa karibu tukio hilo ambalo lilimhusisha muuguzi aliyeshambuliwa akiwa katika utekelezaji wa majukumu yake ya kumhudumia mgonjwa.

“Tumeelezwa kuwa wahusika walifikia hatua ya kuombana msamaha, lakini sisi kama TANNA tunaona ni muhimu kuweka wazi kwa umma na wataalamu wote wa afya kuwa tukio hili ni kubwa zaidi ya mgogoro wa watu wawili,” alisema Dkt. Mbao.

Aliongeza kuwa kitendo hicho kilimdhalilisha muuguzi akiwa katika mazingira yake ya kazi, kikakiuka utu wake na kuhatarisha usalama wake pamoja na wa mgonjwa aliyekuwa akihudumiwa na wagonjwa wengine waliokuwapo eneo la tukio.

Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Wauguzi Tawi la Hospitali ya Benjamin Mkapa, Mwabu Thobias, aliziomba mamlaka kuhakikisha sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyowekwa inazingatiwa ili kulinda usalama na wakati mwingine uhai wa wauguzi ambao ni kundi kubwa la watumishi wanaotoa huduma za afya nchini.

“Ni muhimu changamoto zinazotokea katika maeneo yetu ya kazi zisitafuniwe ufumbuzi kwa kuzificha. Tunapaswa kuzizungumza na kuzishughulikia kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo,” alisema Thobias.

Aidha, TANNA imewakumbusha wananchi na wauguzi nchini kuwa vitendo vya kushambuliana, unyanyasaji na ukatili katika maeneo ya kazi ni makosa ya jinai na kwamba sheria zinapaswa kuchukua mkondo wake bila kuangalia taaluma au cheo cha mhusika.

Miongoni mwa maazimio yaliyotolewa na chama hicho ni kuendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya tukio hilo hadi hatua stahiki zitakapochukuliwa.

No comments:

Post a Comment