
Na Mwandishi Wetu, WMJJWM Dar Es Salaam
Serikali ya Tanzania na Ujerumani zimesaini Makubaliano ya Utekelezaji wa Mradi wa Kituo cha Mabadiliko ya Kidijitali Tanzania (Digital Transformation Centre – DTC Tanzania), utakayochochea ushiriki wa wanawake na wasichana katika uchumi wa kidijitali kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini baina ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ujerumani (GIZ) iliyofanyika jijini Dar es Salaam Juni 11, 2026, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Bw. Badru Alburnoor amesema makubaliano hayo yanafungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya nchi ya Tanzania na Ujerumani katika kuhakikisha wanawake na wasichana wanapata fursa sawa za kushiriki na kunufaika na maendeleo ya teknolojia za kidijitali.
Amesema mradi huo unaendana kikamilifu na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Jinsia na Wanawake ya mwaka 2023, Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto pamoja na Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali wa mwaka 2024–2034.
“Teknolojia za kidijitali zimekuwa nyenzo muhimu katika kubadilisha namna wananchi wanavyojifunza, kufanya kazi, kupata huduma na kushiriki katika shughuli za maendeleo. Serikali inaona umuhimu wa kuhakikisha wanawake na wasichana hawabaki nyuma katika mabadiliko haya, bali wanakuwa sehemu ya nguvu kazi na wabunifu wa teknolojia zinazochochea maendeleo ya taifa,” amesema Alburnoor.
Ameongeza kuwa kabla ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, Wizara kwa kushirikiana na GIZ tayari imefanikiwa kutekeleza programu mbalimbali zilizolenga kukuza ushiriki wa wanawake katika sekta ya teknolojia, kuimarisha ujuzi wa kidijitali na kuhamasisha ubunifu unaotumia teknolojia katika kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi.
Kwa mujibu wa Alburnoor, Mradi wa DTC Tanzania unalenga kuendeleza suluhisho za kidijitali zinazobuniwa ndani ya nchi huku ukijenga mazingira jumuishi ya ushiriki katika uchumi wa kidijitali kwa kuimarisha ujuzi wa kidijitali, mifumo ya ubunifu na matumizi ya teknolojia zinazoboresha maisha ya wanawake na wasichana.
Amefafanua kuwa utekelezaji wa mradi huo utajikita katika maeneo matatu makuu, ikiwemo kuandaa mkakati wa Wizara wa kuimarisha usawa wa kijinsia unaozingatia fursa na changamoto za matumizi ya teknolojia za kidijitali, kuwajengea uwezo wawakilishi 200 kutoka taasisi za Serikali na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutumia mbinu za kidijitali katika shughuli zao za kila siku, pamoja na kuwafikia Watanzania 100,000 kupitia suluhisho za kidijitali zinazokuza usawa wa kijinsia na haki za binadamu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZA ) Anne Hahn amesema GIZ kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania inaendelea na maandalizi ya kuanzisha Maabara ya Ubunifu wa Kidijitali (Digital Fabrication Lab) pamoja na Kituo cha Ubunifu na Utengenezaji Teknolojia (Makerspace) kitakachohifadhiwa katika Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO).
Alisema vituo hivyo vitatoa fursa kwa wanawake na wasichana kupata mafunzo ya vitendo kuhusu teknolojia zinazoibuka, kutumia vifaa vya kisasa vya kidijitali na kushiriki katika ubunifu wa teknolojia unaoweza kuzalisha ajira na kuongeza kipato.
“Lengo letu ni kuwawezesha wanawake na wasichana kuhama kutoka kuwa watumiaji wa teknolojia pekee na kuwa wabunifu, wavumbuzi na wajasiriamali wa teknolojia watakaotoa mchango mkubwa katika uchumi wa kidijitali wa Tanzania,” amesisitiza.
Naye Mkuuwa Mahusiano Ubalozi wa Ujerumani nchini amebainisha kuwa mafanikio ya mabadiliko ya kidijitali yanahitaji ushirikiano mpana wa wadau mbalimbali, hivyo Wizara itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi za umma, mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi za elimu na utafiti, vituo vya ubunifu pamoja na sekta binafsi.
Amesema ushirikiano huo utawezesha Tanzania kujenga jamii inayonufaika kwa usawa na maendeleo ya teknolojia, huku ikiimarisha ushirikishwaji wa wanawake na makundi mengine maalum katika shughuli za maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Makubaliano hayo yanatarajiwa kuwa chachu ya kuongeza ushiriki wa wanawake katika sekta ya teknolojia nchini na kuchangia utekelezaji wa ajenda ya Taifa ya kujenga uchumi wa kidijitali unaojumuisha wananchi wote bila ubaguzi.








No comments:
Post a Comment