TANZANIA NA UTURUKI KUIMARISHA BIASHARA NA MAENDELEO YA VIWANDA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, June 7, 2026

TANZANIA NA UTURUKI KUIMARISHA BIASHARA NA MAENDELEO YA VIWANDA


Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga, akiwa katika ziara ya kikazi nchini Uturuki Juni 06, 2026, Jijini Istanbul amefanya mazungumzo na Waziri wa Viwanda na Teknolojia wa Uturuki, Mehmet Fatih Kacır pamoja na Waziri wa Biashara wa Uturuki, Ömer Bolat, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na viwanda kati ya nchi hizi mbili.

Mazungumzo na Waziri Kacır yamejikita katika kukuza maendeleo ya viwanda vya kimkakati, kuimarisha matumizi ya teknolojia, pamoja na kuhamasisha uwekezaji katika viwanda rafiki kwa mazingira.

Mhe. Kapinga ameeleza dhamira ya serikali ya kutumia ushirikiano huo kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya mwaka 2050 ya kuwa nchi ya kipato cha kati cha juu kupitia mageuzi ya sekta ya viwanda, huku Uturuki ikiahidi kuendeleza ushirikiano wa kiufundi, kiteknolojia na ubunifu kwenye sekta hiyo.

Kwa upande wa biashara, mazungumzo na Waziri Bolat yamejikita katika kuimarisha mazingira wezeshi ya uwekezaji na kuongeza kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Uturuki, ambacho kwa sasa kimefikia takribani Dola za Marekani milioni 354 mwaka 2026, huku lengo likiwa ni kufikia Dola za Marekani bilioni moja.

Pande zote mbili zilikubaliana kuandaa Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Biashara utakaofanyika nchini Tanzania mwaka 2026 ili kujadili kwa kina fursa za kibiashara na uwekezaji.

Waziri Kapinga ametumia fursa hiyo kuelezea maeneo ya kimkakati ya uwekezaji nchini Tanzania, yakiwemo viwanda vya chuma, dawa na vifaa tiba, chakula, pamoja na kongani za viwanda vya kijani (green industrial parks), akisisitiza umuhimu wa kuongeza thamani ya malighafi za kilimo na madini ili kukuza ajira na kuongeza mauzo ya bidhaa zilizochakatwa badala ya kuuza malighafi ghafi.

Serikali ya Uturuki imeahidi kuendeleza ushirikiano wa kimkakati na Tanzania kupitia ubadilishanaji wa teknolojia, ujuzi na kuhamasisha sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika miradi ya maendeleo ya viwanda.


Aidha, Waziri Kapinga alifanya mazungumzo na Waziri wa Biashara wa Somalia, Gamal Hassan, ambapo walijadili umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kupitia biashara na uwekezaji ili kunufaika vema na fursa za soko la Afrika Mashariki. Vilevile, kupitia mazungumzo hayo Mawaziri hao wameazimia kuanzisha makongamano ya biashara yatakayozikutanisha taasisi za serikali, wafanyabiashara na sekta binafsi kujadili kwa pamoja masuala muhimu ya ushirikiano.

Kadhalika, Mawaziri hao walijadili umuhimu wa uanzishwaji wa safari za ndege kati ya Tanzania na Somalia kupitia Shirika la Ndege la Air Tanzania ili kurahisisha usafirishaji na kupanua mtandao wa biashara kati ya nchi hizi mbili. Waziri Kapinga alihitimisha mazungumzo hayo kwa kumshukuru Waziri Hassan na alimuhakikishia utayari wa Tanzania kuimarisha uhusiano na Somalia na aliwakaribisha wawekezaji kutoka nchini humo kuja kuwekeza Tanzania.

No comments:

Post a Comment