TUCTA, ILO WAZINDUA KITUO CHA MSAADA KWA WAFANYAKAZI WAHAMIAJI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, June 11, 2026

TUCTA, ILO WAZINDUA KITUO CHA MSAADA KWA WAFANYAKAZI WAHAMIAJI

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) kwa kushirikiana na Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa (ILO) limezindua Kituo cha Msaada kwa Wafanyakazi Wahamiaji Tanzania (TUCTA-MWRC) kwa lengo la kuwapatia taarifa, ushauri na msaada wafanyakazi wanaotafuta ajira ndani na nje ya nchi.

Akizungumza leo Juni 11, 2026 katika hafla ya uzinduzi wa kituo hicho iliyofanyika Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa ILO Kanda ya Afrika Mashariki, Caroline Mugalla, amesema kituo hicho kimeanzishwa ili kusaidia kulinda haki na maslahi ya wafanyakazi wahamiaji kwa kuwapatia taarifa sahihi, mwongozo na huduma mbalimbali zinazohusiana na uhamiaji wa kazi.

Amesema huduma hizo zitatolewa kwa Watanzania wanaotafuta ajira nje ya nchi pamoja na wafanyakazi wa kigeni wanaokuja kufanya kazi nchini, hatua inayolenga kuhakikisha uhamiaji wa wafanyakazi unafanyika kwa usalama na kwa kuzingatia haki za binadamu.

“Uhamiaji wa wafanyakazi unapofanyika kwa usalama na kwa kuzingatia haki za binadamu, unachangia ukuaji wa uchumi, kuongeza tija, kuhamasisha uhamishaji wa ujuzi na kuleta maendeleo,” amesema Mugalla.

Hata hivyo, amesema wafanyakazi wahamiaji bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo ukosefu wa taarifa sahihi kuhusu ajira wanazokwenda kufanya, mikataba isiyoeleweka, gharama kubwa za uhamiaji na vitendo vya unyonyaji vinavyojitokeza katika baadhi ya maeneo ya ajira.

Ameeleza kuwa changamoto hizo zimekuwa zikiwasukuma baadhi ya wafanyakazi kuingia katika mazingira hatarishi ya kazi, hali inayodhihirisha umuhimu wa kuimarisha mifumo ya ulinzi wa haki zao na upatikanaji wa taarifa sahihi kabla ya kusafiri.

Mugalla amesema kituo hicho kitachangia kukuza uhamiaji salama unaozingatia sheria na viwango vya kazi vinavyotambulika kimataifa, sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kulinda haki za wafanyakazi.

“Taarifa sahihi zitawasaidia wafanyakazi kufanya maamuzi sahihi na kujikinga dhidi ya udhalilishaji na aina mbalimbali za unyonyaji,” amesema.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa TUCTA, Shaban Ambindwile, amelishukuru ILO kwa kuendelea kushirikiana na shirikisho hilo katika kuimarisha ulinzi wa wafanyakazi na kuboresha mazingira ya kazi kwa Watanzania wanaotafuta ajira nje ya nchi.

Amesema kituo hicho kitakuwa msaada mkubwa kwa wafanyakazi kwa kuwapatia taarifa, ushauri na msaada wanapokumbana na changamoto mbalimbali wakiwa nje ya nchi.

“Lengo letu ni kuisaidia Serikali kuhakikisha wafanyakazi wetu wanakuwa salama na wanapata msaada wanapokumbana na changamoto mbalimbali wakiwa nje ya nchi,” amesema Ambindwile.

Ameongeza kuwa TUCTA itashirikiana na mashirikisho ya wafanyakazi katika nchi mbalimbali ili kurahisisha mawasiliano na utoaji wa msaada kwa Watanzania wanaofanya kazi nje ya mipaka ya nchi.

Aidha, amesema wakati Serikali ikiendelea kutafuta fursa za ajira katika masoko ya kimataifa, kituo hicho kitakuwa na jukumu la kufuatilia mazingira ya kazi na ustawi wa Watanzania wanaopelekwa kufanya kazi nje ya nchi.

Naye Ofisa Kazi Mwandamizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Oddo Hekela, amesema uzinduzi wa kituo hicho ni hatua muhimu katika kuimarisha usalama wa Watanzania wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi.

Amesema kituo hicho kitakuwa daraja muhimu kati ya wafanyakazi, Serikali na wadau wengine kwa kutoa taarifa zinazohusu ajira, vibali vya kazi na masuala mengine ya uhamiaji.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM), Valda Chali, amesema uzinduzi wa kituo hicho umefanyika wakati mwafaka kutokana na kuongezeka kwa uhamaji wa wafanyakazi ndani na nje ya ukanda wa Afrika Mashariki.

Amesema wahamiaji wengi bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo taarifa potofu, unyonyaji katika mchakato wa ajira, biashara ya binadamu na ukosefu wa huduma za msaada.

“IOM tumekuwa tukishirikiana kwa karibu na Serikali ya Tanzania pamoja na wadau wengine kuimarisha mifumo ya usimamizi wa ajira za wahamaji na kuhamasisha ajira zenye maadili kupitia Mfumo wa Kimataifa wa Uadilifu katika Uajiri (IRIS),” amesema Chali.

Takwimu za ILO zinaonyesha kuwa mwaka 2022 kulikuwa na wafanyakazi wahamiaji milioni 167.7 duniani, sawa na asilimia 4.7 ya wafanyakazi wote duniani, ambapo wanaume walikuwa milioni 102 na wanawake milioni 64.9. Hali hiyo inaonesha umuhimu wa kuendelea kuimarisha mifumo ya ulinzi na usaidizi kwa wafanyakazi wahamiaji duniani.

No comments:

Post a Comment