TUME YA MADINI YAHAMASISHA UWEKEZAJI KUPITIA MAONESHO YA UBUNIFU IRINGA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, June 4, 2026

TUME YA MADINI YAHAMASISHA UWEKEZAJI KUPITIA MAONESHO YA UBUNIFU IRINGA



Na Mwandishi Wetu - IRINGA


Tume ya Madini kupitia Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Iringa imeendelea kuhamasisha uwekezaji katika Sekta ya Madini kwa kutoa elimu na kuonesha fursa mbalimbali zilizopo kupitia Maonesho ya Utafiti, Ubunifu na Huduma kwa Jamii yanayoendelea katika viwanja vya Garden Posta, Manispaa ya Iringa.

Maonesho hayo, yaliyowakutanisha taasisi mbalimbali za serikali na sekta binafsi, yanalenga kuelimisha wananchi kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi hizo pamoja na fursa za kiuchumi zinazopatikana katika maeneo mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo sekta ya madini.

Akizungumza katika maonesho hayo, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Iringa, Mjiolojia Bertha Luzabiko, amesema ushiriki wa Tume ya Madini unalenga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu shughuli za madini, taratibu za upatikanaji wa leseni za madini na fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta hiyo.

Amesema Mkoa wa Iringa una rasilimali mbalimbali za madini zenye mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi, hivyo wananchi na wawekezaji wanapaswa kuzitumia fursa hizo kwa kufuata sheria, kanuni na miongozo inayosimamia sekta ya madini nchini.

Awali akifungua maonesho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, aliwataka wananchi kutumia maonesho hayo kujifunza, kufanya ubunifu na kunufaika na fursa zinazotolewa na taasisi mbalimbali kwa maendeleo yao na ya taifa.

Maonesho hayo yameandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Mkwawa, yakilenga kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za umma, sekta binafsi na wananchi katika kuchochea maendeleo kupitia utafiti, ubunifu na utoaji wa huduma bora kwa jamii.

No comments:

Post a Comment