WANANCHI WATAKIWA KUHESHIMU HAKI ZA WATOTO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, June 17, 2026

WANANCHI WATAKIWA KUHESHIMU HAKI ZA WATOTO


Na. Wellu Mtaki, Dodoma


Wazazi na walezi wamehimizwa kuwalea watoto katika maadili mema ili kuwaepusha na tabia za kuiga zisizofaa ambazo zinaweza kuwaletea madhara katika maisha yao. 

Sambamba na hilo, wananchi wametakiwa kutambua na kuheshimu haki za watoto ili kuhakikisha wanakua katika mazingira salama na yenye upendo.

Kauli hiyo imetolewa na Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Faithmary Lukindo, alipokuwa akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Eliakim Chacha Maswi, katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika katika Kituo cha Malezi ya Watoto Kikombo jijini Dodoma.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo viongozi wa kijiji, viongozi wa dini, wastaafu pamoja na waimbaji wa Kwaya ya Gethsemane.

Akizungumza katika hafla hiyo, Lukindo alisema mtoto anapopewa haki ya kusikilizwa na kutoa maoni yake, hujengewa hali ya kujiamini na kujiona mwenye thamani ndani ya familia na jamii inayomzunguka.

“Kumpatia mtoto haki ya kusikilizwa kwa kutoa maoni yake kunamsaidia kujiamini na kujiona mwenye thamani katika familia na hata katika jamii anayoishi. Hivyo wazazi na walezi wanapaswa kuwapa watoto wao fursa hiyo,” alisema.

Aidha, alieleza kuwa serikali kupitia wizara itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuendeleza ustawi wa watoto, akisisitiza kuwa watoto ndio msingi wa maendeleo ya taifa la kesho.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Jukwaa la Haki za Watoto Tanzania, Sylvia Ruambo, alitoa wito kwa jamii kuendelea kuwalinda na kuwapenda watoto, akibainisha kuwa watoto wote wana haki sawa zinazopaswa kuheshimiwa na kulindwa.

“Tunaomba jamii iendelee kuwalinda na kuwapenda watoto kwani wote wana haki sawa. Sisi kama Bodi tutakuwa mstari wa mbele kutetea na kulinda maslahi yao,” alisema.

Naye Askofu wa Kanda ya ECM Bethel, Richard Mwalyego, alisema kuanzishwa kwa mradi wa saluni katika Kituo cha Malezi ya Watoto Kikombo ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha watoto kupata ujuzi wa kujitegemea utakao wanufaisha katika maisha yao ya baadaye.

Alifafanua kuwa kituo hicho kinaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo yenye lengo la kugusa mahitaji ya jamii na kuwajengea watoto uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha.

“Mradi huu wa saluni umeanzishwa kwa lengo la kuwapatia watoto ujuzi utakaowasaidia kujitegemea na kuwaepusha na vishawishi viovu vinavyoweza kuharibu maisha yao,” alisema.

Aidha, aliwataka wazazi kuhakikisha wanawalea watoto katika misingi ya maadili na imani njema ili kuwajengea msingi bora wa maisha yao ya baadaye.

Kwa niaba ya Afisa Elimu Kata ya Hombolo, mwalimu aliyemwakilisha alisema serikali inaendelea kuweka juhudi kubwa katika kuhakikisha watoto wanatimiza ndoto zao kupitia sekta ya elimu. Aliongeza kuwa walimu wana wajibu wa kuongeza bidii katika kuwalea na kuwafundisha watoto ili wafikie malengo yao.

“Serikali inaendelea kupambana kuhakikisha watoto wanatimiza ndoto zao. Sisi walimu tuna wajibu wa kuongeza juhudi ili kuwasaidia kufikia malengo yao na kuwa raia bora wa baadaye,” alisema.

Awali, Mkurugenzi wa Kituo cha Malezi ya Watoto Kikombo, Darius Kalijongo, alisema kituo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali za kitabia zinazotokana na watoto kutoka mazingira tofauti ya kijamii.

Alisema ili kukabiliana na changamoto hizo, kituo kimeweka mifumo ya uangalizi ikiwemo kamera za usalama katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuzuia vitendo viovu na kuimarisha malezi.
“Changamoto ya kitabia ni miongoni mwa changamoto kubwa tunazokabiliana nazo.

Ndiyo maana tumeimarisha mifumo ya uangalizi ili kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira salama,” alisema.

Pia alibainisha kuwa kituo hicho kinaendesha miradi mbalimbali ya uzalishaji ambayo imekuwa ikichangia upatikanaji wa chakula na kuboresha ustawi wa watoto wanaolelewa hapo.

Maadhimisho hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kuikumbusha jamii wajibu wake wa kulinda, kulea na kuendeleza haki za watoto, ambao ndiyo nguzo ya maendeleo endelevu ya taifa. 

No comments:

Post a Comment