WAZIRI MASAUNI ASITISHA SHUGHULI ZA KIWANDA CHA AFRICAN STEEL KWA UCHAFUZI WA MAZINGIRA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, June 27, 2026

WAZIRI MASAUNI ASITISHA SHUGHULI ZA KIWANDA CHA AFRICAN STEEL KWA UCHAFUZI WA MAZINGIRA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Masauni, amesitisha shughuli za Kiwanda cha African Steel Group Company Limited kilichopo Kijiji cha Mwavi, Kata ya Fukayosi, Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, kinachotumia chuma chakavu kuzalisha nondo kwa ukiukwaji wa Sheria na Kanuni za uhifadhi wa mazingira.

Hatua hiyo imefikiwa wakati wa ziara ya Waziri Masauni ya kukagua utekelezaji wa Sheria za mazingira katika viwanda vitatu vilivyopo Wilaya ya Bagamoyo, ambapo amekipongeza kiwanda cha KAMAL Refinery Limited kinachojishughulisha na uchakataji wa mafuta machafu na Roster Vehicle Equipment Limited kinachojihusisha na utengenezaji na uunganishaji wa magari (truck assembly) kwa Usimamizi mzuri wa Sheria ya Mazingira

Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Waziri Masauni amesema Kiwanda cha African Steel kimeendelea kuchafua mazingira licha ya kupewa maelekezo mara kadhaa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kufuatia ukaguzi uliofanyika lakini kimepuuza na kushindwa kuyatekeleza, hali iliyoilazimu Serikali kuchukua hatua ya kusitisha shughuli zake.

Ametaja ukiukwaji uliobainika kuwa ni uchafuzi mkubwa wa hewa unaotokana na moshi mzito unaohatarisha afya za wafanyakazi na wananchi, utiririshaji wa majitaka kwenye mazingira, utupaji holela wa taka pamoja na kukosekana kwa eneo maalumu la kuhifadhi chuma chakavu, hali inayosababisha uchafuzi wa ardhi. Kutokana na hali hiyo, ameamuru shughuli za kiwanda hicho kusitishwa hadi kitakapotekeleza kikamilifu maelekezo ya NEMC na Serikali.

Aidha, Waziri Masauni ameipongeza NEMC kwa kazi kubwa ya ukaguzi na usimamizi wa mazingira nchini, huku Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Dkt. Immaculate Sware Semesi akiahidi kuendelea kusimamia kikamilifu Sheria ya Mazingira katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuhakikisha viwanda vinazingatia matakwa ya kisheria.

Waziri Masauni amesisitiza kuwa lengo la Serikali si kusitisha uwekezaji, bali kuhakikisha shughuli zote za uzalishaji zinafanyika kwa kuzingatia sheria, kulinda afya za wananchi na kuhifadhi mazingira kwa maendeleo endelevu.

No comments:

Post a Comment