Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius J. Ndejembi (Mb.), amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu kuunda kamati ya uchunguzi itakayobaini chanzo cha hitilafu iliyojitokeza katika Gridi ya Taifa jana, Juni 27, 2026, na kusababisha kukosekana kwa huduma ya umeme katika maeneo mbalimbali nchini, ili kuwezesha kuchukuliwa kwa hatua za haraka na kuhakikisha tatizo hilo halijitokezi tena.
Waziri Ndejembi ametoa maelekezo hayo leo, Juni 28, 2026, Ubungo jijini Dar es Salaam katika Kituo cha usimamizi wa Gridi ya Taifa, ambapo ameelekeza kamati hiyo ishirikishe wataalamu kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama, ikiwa na jukumu la kufanya uchunguzi wa kina na kupendekeza hatua za kudumu za kuzuia matukio kama hayo kujirudia.
Waziri Ndejembi amemtaka Mtendaji Mkuu wa TANESCO kuwasilisha taarifa ya awali ndani ya wiki moja ili kuiwezesha Serikali kuchukua hatua za haraka, wakati Kamati ikiendelea na uchunguzi wa kina.
Aidha, Waziri Ndejembi ameiagiza TANESCO kuimarisha mfumo wa Gridi ya Taifa kwa kuweka mifumo madhubuti ya ulinzi na udhibiti ili hitilafu zinazotokea katika eneo moja zisisababishe athari kwa mfumo mzima wa usambazaji wa umeme nchini.
“Kilichokatika jana ni gridi ya Taifa, sio usalishaji wa umeme. Uzalishaji hauna changamoto yoyote lakini baada ya gridi kukatika ilisababisha mitambo ya uzalishaji kuzima kwani ni mitambo ya kisasa” amesema Ndejembi
Waziri Ndejembi amesisitiza umuhimu wa kukamilisha kwa wakati miradi ya kimkakati ya njia za kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 400, ikiwemo Chalinze – Kinyerezi na Chalinze – Dodoma, akieleza kuwa ukamilishaji wake utaongeza uthabiti na usalama wa mfumo wa Gridi ya Taifa.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Felchesmi Mramba, amesema Wizara itasimamia kikamilifu utekelezaji wa maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri, ikiwemo kazi ya Kamati ya Uchunguzi na utekelezaji wa miradi ya kuimarisha Gridi ya Taifa.
“Tutaimarisha usimamizi wa utekelezaji wa maelekezo haya na kufuatilia kwa karibu miradi ya njia za kusafirisha umeme ili ikamilike kwa wakati, hatua itakayoongeza uthabiti na ufanisi wa Gridi ya Taifa,” amesema Mhandisi Mramba.









No comments:
Post a Comment