WIZARA YA ELIMU YATANGAZA NAFASI ZA MAFUNZO YA UALIMU KWA MWAKA WA MASOMO 2026/2027 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, June 11, 2026

WIZARA YA ELIMU YATANGAZA NAFASI ZA MAFUNZO YA UALIMU KWA MWAKA WA MASOMO 2026/2027


Na Mwandishi Wetu


WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetangaza rasmi nafasi za mafunzo ya Ualimu ngazi ya Stashahada ya Elimu ya Awali na Msingi kwa mwaka wa masomo 2026/2027, hatua inayolenga kuongeza idadi ya walimu wenye sifa stahiki na kuimarisha ubora wa elimu nchini.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Carolyne Nombo, mafunzo yatakayopatikana ni pamoja na Stashahada ya Ualimu Elimu ya Awali na Msingi ya miaka miwili, Stashahada Maalumu ya Ualimu Elimu ya Msingi katika masomo ya Sayansi na Hisabati ya miaka mitatu, pamoja na Stashahada ya Ualimu Elimu ya Awali na Msingi kwa njia ya masafa inayochukua kati ya miaka mitatu hadi minne.

Tangazo hilo limeeleza kuwa mafunzo hayo yatatolewa katika vyuo vya ualimu vya Serikali na vile visivyo vya Serikali vilivyopata idhini ya kuendesha programu husika.

Kwa upande wa sifa za kujiunga, wahitimu wa Kidato cha Sita wenye ufaulu wa Principal Pass mbili katika daraja la I hadi III wanastahili kuomba mafunzo ya Stashahada ya Ualimu Elimu ya Awali na Msingi ya miaka miwili.

Pia walimu waliomaliza mafunzo ya Astashahada ya Ualimu Elimu ya Awali au Msingi wanaruhusiwa kuomba.

Aidha, kwa mafunzo maalumu ya miaka mitatu katika masomo ya Sayansi na Hisabati, waombaji wanatakiwa kuwa wahitimu wa Kidato cha Nne wenye alama za “C” au zaidi katika masomo husika ya sayansi na hisabati.

Wizara imebainisha kuwa waombaji wa vyuo vya Serikali wanapaswa kutuma maombi yao kwa njia ya mtandao kupitia mfumo wa udahili wa walimu, huku waombaji wa vyuo visivyo vya Serikali wakitakiwa kuwasilisha maombi moja kwa moja katika vyuo wanavyovichagua.

Majibu ya waliochaguliwa kujiunga na vyuo vya Serikali yatatolewa kuanzia Julai 15, 2026 kupitia akaunti walizotumia wakati wa kuwasilisha maombi pamoja na katika vyuo walivyopangiwa.

Wizara imewahimiza waombaji kuhakikisha wanaandika anuani sahihi, namba za simu na barua pepe zinazopatikana kwa urahisi ili kurahisisha mawasiliano.

Mwisho wa kutuma maombi umetajwa kuwa ni Julai 10, 2026, ambapo waombaji wote wenye sifa wanahimizwa kutumia fursa hiyo kujiunga na taaluma ya ualimu ambayo ina mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa.

Hatua hiyo inaonesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha sekta ya elimu kwa kuongeza wataalamu wa kufundisha katika ngazi za elimu ya awali na msingi, sambamba na kukidhi mahitaji ya walimu katika maeneo mbalimbali nchini.

No comments:

Post a Comment