CCT YAWEKEZA BILIONI 3.8 DODOMA, RC SENYAMULE APONGEZA MAZINGIRA BORA YA UWEKEZAJI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, July 9, 2026

CCT YAWEKEZA BILIONI 3.8 DODOMA, RC SENYAMULE APONGEZA MAZINGIRA BORA YA UWEKEZAJI



Na Mwandishi Wetu, Dodoma


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amesema Serikali ya Awamu
ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan, imeendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji na kukuza sekta
binafsi, ikiwemo uwekezaji unaofanywa na Taasisi za Dini kutokana na mchango wake
mkubwa katika kukuza uchumi wa Nchi.

Mhe. Senyamule ameyasema hayo leo Julai 09, 2026, wakati wa hafla ya uzinduzi wa
jengo la kitega uchumi la Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT Complex), hafla
iliyoambatana na Mkutano wa 60 wa Halmashauri Kuu ya Jumuiya hiyo, uliofanyika katika
ukumbi uliopo ndani ya jengo hilo.

"Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji na kukuza sekta binafsi,
ikiwemo Taasisi za Dini. Tunatambua mchango mkubwa wa taasisi hizi katika utoaji wa
elimu, huduma za afya, kujenga maadili ya jamii na kuchochea maendeleo ya kiuchumi,"
amesema Mhe. Senyamule.

Ameongeza kuwa miradi ya uwekezaji kama huo ni mfano mzuri wa namna Taasisi za
Dini zinavyoweza kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa Taifa kupitia uanzishaji
wa vitega uchumi vinavyozalisha ajira, kuongeza mapato na kupanua fursa za kiuchumi
kwa wananchi. Aidha, amesema uwekezaji huo unaakisi maono yenye uwezo wa kuleta
mabadiliko chanya katika maisha ya watu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCT, Askofu Dkt. Stanley Hotay, amesema uwekezaji
huo ni hatua muhimu katika safari ya Jumuiya hiyo kuelekea kujitegemea na kupunguza
utegemezi wa misaada kutoka nje.

Amesema kupitia uwekezaji huo, CCT imeongeza
uwezo wake wa kuzalisha mapato ya ndani, ambapo hadi kufikia Juni 2026 kiwango cha
kujitegemea kimeongezeka hadi asilimia 33 kutoka asilimia 20 iliyokuwepo wakati wa
tathmini ya awali mwaka 2025.

Naye Katibu Mkuu wa CCT, Mchungaji Canon Dkt. Moses Matonya, amesema jengo hilo
la uwekezaji linaisaidia Jumuiya kujijengea uwezo wa kifedha, huku likichangia pia
kuwahudumia wananchi kupitia kuimarisha shughuli za uinjilishaji katika maeneo
mbalimbali ya Nchi pamoja na utoaji wa huduma za kijamii zinazotekelezwa na Jumuiya
hiyo.

Mradi wa ujenzi wa jengo la kitega uchumi la CCT ulianza mwaka 2023 na unatarajiwa
kukamilika mwaka 2026. Umegharimu shilingi bilioni 3.8 na hadi sasa umefikia asilimia
95 ya utekelezaji. Jengo hilo linatarajiwa kuingiza mapato ya takribani shilingi milioni 600 kwa mwaka, huku likiwa na uwezo wa kuhudumia zaidi ya watu 500 katika kumbi zake.




No comments:

Post a Comment