
Mkuu wa wilaya ya Bahi Mhe. Joachim Thobias Nyingo amekabidhi gari jipya aina ya ‘Toyota Pickup’ kwa Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wa wilaya hiyo Mha. Hopeness Liundi huku akitoa wito wa kutumia vizuri kitendea kazi hicho kwa kuongeza kasi ya utendaji kazi kwa tija ili kufikia lengo la kumtua mama ndoo kichwani kwa kuwafikishia huduma ya Majisafi ya bomba wananchi wa wilaya hiyo.
Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika katika ofisi ya Meneja RUWASA Mkoa wa Dodoma Julai 27, 2026 na kuhudhuriwa na Meneja wa Mkoa huo Mha. Beatrice Kasimbazi pamoja na watumishi wengine wa mkoa huo.
Akizungumza kabla ya kuzindua na kukabidhi gari hilo, Mhe. Nyingo aliishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuiwezesha RUWASA na kuboresha utendaji wao wa kazi ikionesha dhamira ya dhati ya serikali kuwafikishia wananchi huduma muhimu ya majisafi ya bomba.
Hivi karibuni, Serikali kupitia RUWASA ilinunua na kugawa magari 22 katika mikoa na wilaya mbalimbali nchini ikiwa ni hatua ya kuboresha na kuimarisha utendaji wa taasisi katika kusimamia na kufuatilia miradi na huduma ya maji katika maeneo ya vijijini.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mkuu wa wilaya Nyingo amemkaribisha Meneja mpya wa RUWASA wa mkoa wa Dodoma Mha. Beatrice Kasimbazi ambaye amehamishiwa mkoani humo akitokea mkoa wa Pwani, huku akitoa wito kwa watumishi wa wilaya hiyo kumpokea na kumpa ushirikiano katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya serikali na kuwahudumia wananchi.









No comments:
Post a Comment