DC NKINDA ASIKILIZA KERO ZA WANANCHI MBULU, AAGIZA HATUA ZA HARAKA KUTATUA MIGOGORO YA ARDHI NA MIUNDOMBINU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, July 28, 2026

DC NKINDA ASIKILIZA KERO ZA WANANCHI MBULU, AAGIZA HATUA ZA HARAKA KUTATUA MIGOGORO YA ARDHI NA MIUNDOMBINU


Na Neema Nkumbi, Kahama


Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, amekutana na wananchi wa Mtaa wa Mbulu, Kata ya Mhongolo, Manispaa ya Kahama, katika mkutano wa hadhara uliolenga kusikiliza kero zao na kuelekeza hatua za kuzitatua, huku akisisitiza uwajibikaji wa viongozi na watendaji wa Serikali katika kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi.


Katika mkutano huo, wananchi waliwasilisha kero mbalimbali zikiwemo migogoro ya ardhi inayodaiwa kusababishwa na upimaji wa viwanja, uharibifu wa miundombinu ya barabara, ukosefu wa maeneo ya huduma za jamii pamoja na madai ya ucheleweshaji wa utatuzi wa migogoro iliyodumu kwa miaka kadhaa.


Akizungumza baada ya kusikiliza malalamiko hayo, Nkinda aliwataka wananchi kutoficha changamoto wanazokutana nazo, bali kuzifikisha kwenye mamlaka husika mapema ili zipatiwe ufumbuzi.


"Msisubiri mpaka viongozi waje ndipo mseme, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ipo, ofisi ya Mkurugenzi ipo, viongozi wa kata na mtaa wapo. Serikali ipo kwa ajili ya kuwasikiliza na kutatua changamoto zenu," amesema Nkinda.


Amesisitiza kuwa viongozi wa Serikali wana wajibu wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa haki na kwamba kutoridhika kwa wananchi kunatokana na kushindwa kushughulikiwa kwa kero zao kwa wakati.


Katika mjadala wa ardhi, wananchi wengi wameeleza kuwa zoezi la upimaji wa viwanja lilisababisha migogoro ya mipaka, baadhi ya maeneo ya barabara kuvamiwa kwa ujenzi, huku wengine wakidai kupoteza sehemu ya ardhi zao na kushindwa kupata namba za viwanja licha ya kupita miaka kadhaa tangu urasimishaji ufanyike.


Wananchi pia waliiomba Serikali kufanya uchunguzi wa kina kuhusu malalamiko yanayohusu usimamizi wa upimaji wa ardhi na kuhakikisha migogoro hiyo inatatuliwa kwa haki.

Akijibu hoja hizo, Mpima Ardhi wa Manispaa ya Kahama Gennadio John amesema upimaji wa Mbulu ulifanywa kwa mfumo wa ushirikishwaji kupitia kampuni ya Geoplan, kwa kushirikiana na kamati za maeneo na wananchi.


Ameeleza kuwa baada ya utekelezaji wa zoezi hilo yalijitokeza malalamiko ya maeneo kuingiliana na changamoto nyingine za mipaka, na kwamba Serikali imekuwa ikipokea malalamiko hayo na kuyafanyia kazi kwa kurejea upimaji katika maeneo yenye migogoro.


Mbali na ardhi, wananchi waliwasilisha pia changamoto za barabara, wakieleza kuwa baadhi ya maeneo yanashindwa kupitika hasa wakati wa mvua.


Kuhusu suala hilo, Nkinda amekiri kuwa Wilaya ya Kahama bado ina changamoto za miundombinu kutokana na asili ya udongo wa maeneo mengi kuwa wa kichanga, hali inayosababisha barabara kuharibika mara kwa mara.


Hata hivyo, amewataka viongozi wa mtaa kushirikisha wananchi na wadau wa maendeleo kutafuta suluhisho la muda wakati Serikali ikiendelea kutafuta fedha za kuboresha miundombinu hiyo.


Aidha, amemwagiza Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbulu kuitisha mkutano wa wananchi na kuwasilisha ndani ya wiki mapendekezo ya hatua za pamoja zitakazosaidia kupunguza changamoto za barabara katika eneo hilo.

Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi wa Serikali, wakuu wa taasisi mbalimbali na wananchi wa Mtaa wa Mbulu, ukiwa sehemu ya utaratibu wa Mkuu wa Wilaya wa kuendelea kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kahama.

No comments:

Post a Comment