Na: OWM (KAM)– Muleba, Kagera
Serikali imesema itaendelea kushirikiana na taasisi za dini katika kuimarisha utoaji wa huduma za kijamii na kujenga jamii yenye maadili, amani na mshikamano huku ikizipongeza kwa mchango wake mkubwa katika kukuza maendeleo ya Taifa.
Kauli hiyo imetolewa leo 4 Julai, 2026 na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Dkt. Eveline Wilbard Munisi alipomwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, katika Harambee ya Ujenzi wa Kanisa la KKKT Usharika wa Ndolage Wilaya ya Muleba mkoani Kagera.
Akizungumza katika hafla hiyo Dkt. Munisi amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuthamini mchango wa taasisi za dini katika kujenga jamii yenye maadili, mshikamano na maendeleo endelevu Alisema ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za dini ni msingi muhimu wa kuimarisha huduma kwa wananchi na kudumisha amani nchini.
Dkt. Munisi amewapongeza viongozi wa Kanisa Kamati ya Ujenzi na waumini wa Usharika wa Ndolage kwa kujitolea kufanikisha ujenzi wa kanisa hilo akieleza kuwa hadi sasa waumini wamechangia kazi na fedha zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 265.8. Aliwataka waumini kuendelea kujitolea ili kuhakikisha nyumba hiyo ya ibada inakamilika kwa wakati.
Aidha amesema Kanisa linaendelea kuwa nguzo muhimu ya jamii kwa kutoa malezi ya kiroho na maadili, huduma za elimu na afya pamoja na kuwasaidia makundi yenye uhitaji Amesisitiza kuwa pamoja na kujenga nyumba za ibada ni muhimu pia kujenga jamii yenye upendo mshikamano na uwajibikaji ili kudumisha amani na maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Magharibi Baba Askofu Dkt. Abednego Keshomshahara ameishukuru Serikali kwa ushirikiano unaoendelea kati yake na taasisi za dini katika utoaji wa huduma za kijamii ikiwemo elimu afya na huduma nyingine muhimu kwa wananchi Ametoa wito kwa Serikali kuendelea kuimarisha ushirikiano huo ili kuongeza ufanisi wa kuwahudumia wananchi.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Dkt. Abel Nyamahanga akitoa salamu za Mkoa amewapongeza viongozi na waumini wa Kanisa kwa hatua waliyoifikia katika ujenzi wa kanisa hilo Pia amepongeza mahubiri yaliyotolewa wakati wa ibada, akisema yamehimiza waumini kuchangia kwa hiari na kwa moyo wa kujitoa bila kulazimishwa.
Katika risala yao viongozi wa Kanisa wameiomba Serikali kushughulikia ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 4.8 kutoka Kamachumu hadi Hospitali ya Ndolage pamoja na kuongeza watumishi wa afya wanaolipwa kupitia ruzuku ya Serikali.
Akijibu maombi hayo Dkt. Munisi ameahidi kuyawasilisha katika mamlaka husika ili yafanyiwe kazi Aidha amewahamasisha waumini na wadau mbalimbali kuendelea kuchangia ujenzi wa Kanisa la KKKT Usharika wa Ndolage akisisitiza kuwa ushirikiano na mshikamano ni msingi muhimu wa maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.










No comments:
Post a Comment