Na Mwandishi Wetu - Namtumbo, Ruvuma
Kamati ya Ukaguzi ya Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imemwelekeza mkandarasi M/s Hera Construction Co. Ltd kuongeza kasi ya ujenzi wa daraja la Muungano lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma ili mradi huo ukamilike ndani ya muda uliopangwa na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi ya TARURA, Bw. Henry Kaywanga amesema kuwa kipindi cha mvua kazi husimama kutokana na eneo hilo kuwa na mvua kubwa na kusababisha kazi kuchelewa hivyo maelekezo ya Kamati ni kwamba mkandarasi afanye kazi kwa bidii ili mradi ukamilike kabla ya mvua kuanza.
"Kamati inamuelekeza mkandarasi kufunga taa katika eneo la mradi ili kazi ziendelee mchana na usiku, kuongeza idadi ya wafanyakazi pamoja na vifaa vya ujenzi ili kuhakikisha daraja hili linakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa", amesema Bw. Kaywanga.
Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Wilaya ya Namtumbo Mhandisi Fabian Lugalaba amesema daraja la Muungano ni mradi wa kimkakati unaokwenda kumaliza changamoto ya kukatika kwa mawasiliano kati ya vijiji vya Minazini na Muungano hususan wakati wa masika.
Ameeleza kuwa wanafunzi wa shule ya msingi Ukombozi, wananchi pamoja na wafanyabiashara wamekuwa wakikumbwa na adha kubwa ya usafiri kutokana na mafuriko hivyo ujenzi wa daraja hilo utahakikisha mawasiliano yanapatikana mwaka mzima.
"Daraja hili la zege lenye urefu wa mita 30 litakapokamilika litawezesha usafiri na usafirishaji kuwa wa uhakika katika majira yote ya mwaka na hivyo kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa eneo hili", amesema Mhandisi Lugalaba.
Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za kutekeleza miradi ya miundombinu inayogusa maisha ya wananchi na kuondoa vikwazo vya usafiri katika wilaya ya Namtumbo.
Naye, mkazi wa Namtumbo Bw. Said Athumani amesema, kukamilika kwa daraja hilo kutafungua fursa mpya za biashara, kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii na kuimarisha shughuli za kiuchumi kwa kuwa wananchi hawatakabiliwa tena na changamoto ya kukatika kwa mawasiliano wakati wa mvua.
Kamati ya Ukaguzi ya TARURA imehitimisha ziara yake ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika mkoa wa Ruvuma ambapo pia ilitembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja la Mtyangimbole–Mnadani katika wilaya ya Songea.






No comments:
Post a Comment